Ndugu zangu,
Katika kuliangalia kwa
karibu hili la nchi yetu kuweka tozo ya asilimia 18 kwa baadhi ya huduma
za kitalii naiona vita ya kimaslahi iliyoibuka kati ya madalali wa
utalii na Serikali inayoweka msimamo unaoungwa mkono na wazalendo wa
nchi hii.
Ni vita ya kupigania maslahi ya wengi dhidi ya wachache.
Haya ni mapambano
muhimu katika wakati tulio nao ambapo wenye kupigania maslahi ya
kiudalali wameshafanikiwa kusambaza hofu kuwa watalii wanaikimbia nchi
yetu na kwamba tunaelekea kushindwa.
Kenya inayozungumzwa
kuondoa kodi hiyo ni hatua ya hila na kizandiki katika ushindani na
inachangiwa pia na pigo wanalolipata kutoka na ugaidi wa el shabaab na
hofu yenye kuambatana nayo hususan watalii. Inasikitisha sana na hatuna
budi kuwa na mshikamano na jirani zetu wa Kenya katika vita vyao dhidi
ya ugaidi.
Hata hivyo, hilo haliondoi ukweli kuwa kwenye sekta ya utalii Kenya ni washindani wetu.
Kama nchi hatuwezi
kubadilisha maamuzi yetu tuliojiridhisha kuwa ni sahihi kwa vile tu
Kenya wameamua vingine. Hizo ni dalili za kuyumba na kutojiamini kama
taifa.
Naamini, Tanzania kama
nchi bado inavutia watu wengi wa dunia kuja kuitembelea kutokana na
vivutio tulivyo navyo na ambavyo vingine hata mtalii aimalize Kenya yote
hawezi kuviona kama si kuzunguka dunia na mwisho kuambiwa, viko
Tanzania tu.
Naamini pia, kama
mtalii alishaamua kutembelea Tanzania tangu Januari mwaka huu, hawezi
kufuta safari yake kwa sababu ya VAT ya asilimia 18. Vinginevyo, hakuwa
na dhati ya kufunga safari ya kuja Tanzania.
Isipokuwa, naamini
mtalii anaweza kufuta safari yake aliyoipanga tangu Januari kwa tishio
la usalama wake, hata kama ungemuahidi kumuondolea VAT na kumkaribisha
airport na glasi ya bure ya juisi ya ukwaju. Hili ni tatizo kwa wengine,
sisi hatuna kwa sasa na linachangia kutuuza kiutalii.
Ni rai yangu kwa
Serikali, kuwa isikubali kusogea hata hatua moja kutoka msimamo wa sasa.
Tuko kwenye vita na tumezidiwa na wapinzani wetu, kwa kiasi fulani
kwenye propaganda.
Vinginevyo, hata kama itachukua muda, lakini haya ni mapambano sahihi na ya haki kwetu, na uwezo wa kushinda tunao.
Maggid.
|
July 15, 2016
VAT YA UTALII NI VITA YA MADALALI DHIDI YA WAZALENDO
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment