Bw. Ndirosy Mlawa akizungumza katika moja ya mikutano ya chama hicho.
Na Beatrice Lyimo-MAELEZO
Dar es Salaam.
CHAMA cha Viziwi Tanzania
(CHAVITA)chaiomba Serikali kuandaa mkakati wa kuwawezesha walimu wa
lugha ya alama kupata utaalamu wa kuweza kufundisha watoto viziwi
kutumia lugha hiyo.
Mwenyekiti wa chama hicho Bw.
Ndirosy Mlawa aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa
habari leo jijini Dar es salaam kuhusu maadhimisho ya wiki ya viziwi
duniani ambapo kitaifa yanafanyika mkoani Tanga.
Bw. Mlawa alisema kuwa mbali
na hali ya maendeleo ya viziwi kuimarika kutokana na kukua kwa mwamko
katika jamii na Serikali kwa ujumla pamoja na ushiriki wa wadau
mbalimbali katika harakati za watu wenye ulemavu ambao wanakabiliwa na
changamoto mbalimbali ikiwemo kutokuwa na wataalamu wa kufundisha
watoto viziwi nchini.
“Kwa sasa hali ya maendeleo kwa
viziwi inazidi kuimarika kutokana na kukua kwa mwamko katika jamii na
serikali kwa ujumla, ushiriki wa wadau mbalimbali katika harakati za
watu wenye ulemavu umesaidia kuimarisha hali hii tofauti na miaka ya
1990” alisema Bw. Mlawa
Aidha, aliendelea kufafanua
kuwa jamii imekuwa ikiunga mkono juu ya matumizi ya lugha ya alama na
kupenda kujifunza lugha hiyo ya viziwi, pia kumekuwa na baadhi ya
taasisi ambazo zinajali mahitaji ya viziwi na kuchukua hatua ya
utekelezaji wa mahitaji hayo.
Mbali na hayo, Mwenyekiti huyo
alisema kuna changamoto nyingi wazipatazo viziwi kutegemeana na hali
halisi ya mazingira, umri na shughuli wazifanyazo ikiwemo kutofundishwa
kwa lugha ya alama katika ngazi zote za upatikanaji wa elimu.
Vilevile ukosefu wa huduma ya
ukalimani kwenye maeneo na matukio nyeti yanawafanya viziwi kufadhaika
na kuonekana kuwa hawawezi, hawaelewi, wagumu na kutowajibika licha ya
baadhi yao kuwa na taaluma mbalimbali.
Bw. Mlawa aliendela kwa kusema
kuwa kutotambuliwa kirahisi na utamaduni wa kiziwi anayetumia lugha ya
alama na kubambikiwa majina yanayodhalilisha utu ni miongoni mwa
changamoto wanazokumbana nazo katika jamii.
Kwa upande wake Mratibu kutoka
Chama cha Walimu wenye Uziwi Tanzania Francis Mbisso alisema kuwa pamoja
na uwepo wa mikakati, sheria, kanuni na programu zenye matamko chanya
bado utekelezaji wake unasuasua kwa baadhi ya maeneo nchini.
Alisema kuwa shule za viziwi na
vitengo vya viziwi zimekuwa zikikosa ufundishaji wa watoto viziwi kwa
kutumia lugha ya alama ikiwa na sababu kubwa ya walimu kukosa utaalamu
wa lugha hiyo na kutegemea kujifunza kutoka kwa wanafunzi wao.
Mbali na hayo alitoa wito kwa
jamii kwa ujumla wakiwemo waandishi wa habari kujifunza lugha ya alama
ili kuweza kuwasaidia na kuwapasha habari zinazohusu jamii na huduma
nyingine.
Wiki ya viziwi duniani
huadhimishwa kila mwaka mwezi Septemba ikiwa na lengo la kuonyesha
jamii uwezo wa viziwi na kuelemisha jamii changamoto wazipatazo kutokana
na hali ya ulemavu wao na jisni ya kuzishughulikia.
No comments:
Post a Comment