KWA MAONI AU USHAURI E-mail: inocomm2014@gmail.com, PIGA SIMU: 0714555668

www.utt-pid.org


TEMBELEA: www.utt-pid.org

September 30, 2016

UVCCM WAPONGEZA HATUA YA SERIKALI KWA KUWACHUKULIA HATUA MAOFISA WAKE KAGERA

UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), umepongeza hatua  zilizochukuliwa na serikali kuwasimamaisha kazi, kuwakamata na kuwafikisha mahakamani maofisa watano wanaotuhumiwa kufungua akaunti bandia kwa lengo la kuiba fedha za michango ya waathirika wa tetemeko la ardhi mkoani Kagera.
Umoja huo umesema  mashirika mengi ya umma, taasisi za serikali, viwanda na kampuni zilizoanzishwa wakati werikali ya awamu ya kwanza chini ya Baba wa Taifa Hayati  Mwalimu Julius Nyerere kwa lengo la kujenga uchumi na kutanua wigo wa ajira  vilikufa kwa uzembe.
Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka, alisema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Kaimu katibu huyo mkuu alisema ili nidhamu ya uwajibikaji serikalini iweze kuzingatiwa haukana namna nyingine zaidi ya kuwawajibisha wanaokiuka utaratibu na kutengeneza njama za kula fedha zinazotengwa kwa ajili ama ya maendeleo au kusaidia wenye shida kama waathirika wa tetemeko hilo.
Alisema UVCCM inampongeza Rais Dk. John Magufuli na serikali yake na kuitia shime isirudi nyuma badala yake itimiza majukumu na wajibu wa kikatiba na kisheria bila kumfumbia macho mtumishi, kiongozi au hata mzee ambaye huko nyuma alishiriki kwenye ufisadi au uovu.
“UVCCM inavipongeza vyombo vya dola kuwafikisha mahakamani aliyekuwa Ofisa Tawala Mkoa (RAS) wa Kagera, Amantius Msole, aliyekuwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Bukoba Kelvin Makonda, aliyekuwa Mhasibu wa Mkoa Kagera Simbaufoo Swai na Meneja wa CRDB Kagera, Karlo Sendwa,”alisema.
Shaka  alisema kwa kuwa watuhumiwa hao wako mahakamani, UVCCM inaamini utaratibu wa kisheria utachukua mkondo wake. Mahakama ni eneo la utoaji haki, anayetuhumiwa kwa kesi huweza kuingizwa hatiani kwa mujibu wa sheria, kuachiwa huru au kuhukumumiwa  bila shinikizo lolote.
“Utendaji wa serikali katika dhamira ya kukuza dhana ya uwajibikaji, uadilifu, uzalendo na uwazi, usibaki serikalini pekee, UVCCM tunaahidi kila panapo na uchafu ndani ya jumuia kama wizi, ubadhirifu au ukwapuaji wa mali tutapekuwa, watakaobainika watachukuliwa hatua,”alisema.
Shaka alisema juhudi za serikali ya awamu ya kwanza chini ya Mwalimu Nyerere zilipotea kutokana na waliokabidhiwa dhamana kutotimiza wajibu na kusababisha kampuni, viwanda na mashirika ya umma kufilisika na kufa kabisa jambo alilosema halipaswi kujirudia kwenye awamu hii ya sasa.

No comments:

Post a Comment