WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa amesema Serikali imeunda timu ya wataalamu ambao watatoa
ushauri juu ya suala zima la kuhamishia makao makuu Dodoma.
Ametoa kauli
hiyo leo mchana (Jumamosi, Oktoba 1, 2016) wakati akizungumza na
watumishi wa Serikali wa mkoa wa Dodoma, wazee wa mkoa huo,
wafanyabiashara pamoja na viongozi mbalimbali kwenye ukumbi wa mikutano
wa Dodoma (Dodoma Convention Centre).
“Tumeunda timu
ya watu 10 ambao ni wataalamu waliobobea kwenye masuala ya ujenzi wa
miji mikuu, hawa wana uzoefu wa kuangalia makao Makuu ya nchi
yanafananaje. Watakuja Dodoma, wapitie master plan na kisha watapita kwenye maeneo kadhaa ya mji ili waone hali halisi ikoje ndipo watupe maoni yao,” amesema.
“Tunataka
tusirudie kosa la Jiji la Dar es Salaam la kulazimika kubomoa makazi ya
watu kila inapolazimu kufanya uboreshaji wa miundombinu. Hawa watu
watatuambia wapi tunatakiwa tuweke njia nne au sita za magari, wapi
tuweke bustani au wapi tujenge nyumba za ghorofa moja, mbili, tatu au
zaidi,” ameongeza.
Akifafanua
kuhusu miundombinu, Waziri Mkuu amesema timu hiyo pia itatakiwa kutoa
ushauri juu ya wapi ijengwe njia ya malori tu au mahali gani
zinahitajika kujengwa barabara za juu (flyovers) ili kuepusha msongamano
katikati ya mji wa Dodoma.
Bila kutaja
majina ya wajumbe wa timu hiyo, Waziri Mkuu amesema timu hiyo
itaongezewa wataalamu kutoka China na Malaysia ambao nchi zao tayari
zina uzoefu wa kuhamisha makao makuu ya nchi zao zaidi ya mara moja.
Alitumia fursa
hiyo kuwaeleza watumishi juu ya uwepo wa Tume ya Kuboresha Maslahi ya
Wafanyakazi ambayo imekuwa ikifanya kazi tangu mwaka jana. “Kuna vikao
vimekuwa vinafanyika tangu mwaka jana baina ya Serikali na viongozi wa
vyama vya wafanyakazi kwa lengo la kujadili uboreshaji wa maslahi ya
wafanyakazi, na jambo hili linaendelea vizuri,” amesema.
Kuhusu madeni
ya watumishi wa umma, Waziri Mkuu amewasihi watumishi wawe na imani na
Serikali yao kuhusu madeni hayo na kwamba ikimaliza uhakiki unaofanyika
hivi sasa, kila mwenye stahili zake atalipwa.
Katika hatua nyingine,
Waziri Mkuu ameutaka uongozi wa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu
(CDA) ihakikishe inakamilisha upimaji wa viwanja 100,000 kama
ilivyojipangia ili watumishi hao pamoja na wananchi waweze kupatiwa
viwanja haraka iwezekanavyo.
“Nimearifiwa
kuwa mna mpango wa kupima viwanja 100,000 kwa ajili ya kuwapatia
wananchi na watumishi. Kamilisheni utaratibu huo haraka ili watumishi
wapewe viwanja na waweze kujenga nyumba zao za kuishi,” amesema huku
akishangiliwa.
Natambua kuwa mmekubaliana kuanzisha utaratibu wa kuingiza viwanja kwenye mfumo wa kompyuta ili kuepuka double allocation.
Harakisheni zoezi hilo ili kama itawezekana, kabla ya Novemba kazi hiyo
iwe tayari na watu wapatiwe viwanja chini ya mfumo huo mpya,”
amesisitiza.
Kuhusu huduma
za kijamii kama elimu, umeme, maji na masoko, Waziri Mkuu
amewahakikishia watumishi hao kwamba Serikali imeangalia kila eneo na
kuzingatia mapendekezo yaliyotolewa ili kuboresha utoaji wa huduma hizo.
Amewataka watumishi hao wabadilike na wawe tayari kuwapokea watumishi
wenzao watakaowasili kwa awamu kuanzia mwezi huu.
No comments:
Post a Comment