Na Is-haka Omar, Zanzibar.
WAFUASI wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM ) Zanzibar wameshauriwa kufuata nyayo za waasisi wa Chama hicho kwa
kujitolea na kuweka mbele dhana ya uzalendo katika kujenga miundombinu
ya kudumu itakayowasaidia vizazi vya sasa na vijavyo.
Ushauri huo umetolewa na Naibu
Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai wakati akifungua kongamano la
CCM Wilaya ya Kati Unguja, amesema maendeleo yaliyopatikana ndani ya
serikali na chama yametokana na juhudi kubwa zilizofanywa na wazee wa
chama hicho.
Aliwataka wafuasi wa CCM kila mtu
kwa nafasi yake kufanya jambo la maendeleo litakalobaki katika vitabu
na historia ya kumbukumbu za chama ili vizazi vijavyo virithi taasisi
yenye nguvu katika suala la maendeleo na ukuaji wa uchumi.
Vuai alisema waasisi hao wameacha
miundombinu na vitega uchumi mbali mbali vikiwemo miundombinu katika
sekta mbali mbali zikiwemo Afya, Elimu na majumba ya maendeleo yaliyopo
kila mikoa nchini ambayo ni matunda ya waasisi wa muungano na Mapinduzi
ya Zanzibar ya mwaka 1964.
“ Wazee wetu wamefanya mengi
ambayo ndiyo tunayojivunia kwa sasa katika nyanja mbali mbali za
kiuchumi, kijamii na kisiasa, hivyo nasaha zangu na sisi tukiwa Wana CCM
wa zama hizi lazima tubuni mambo mapya yatakayowanufaisha vizazi
vijavyo.”, alieleza Vuai na kuongeza kuwa CCM mpya itajengwa na fikra
mpya zitakazosaidia kuinua maendeo ya chama.
Akizungumzia miaka 40 ya kuzaliwa
kwa Chama hicho alisema wananchi wa mijini na vijijini wameweza
kunufaika na fursa mbali mbali zinazotokana na sera za chama.
Alisema wakati CCM inazaliwa
mwaka 1977 ASP ilikuwa na miaka 20 na CCM imetimiza miaka 40 ambayo kwa
ujumla wake ni miaka 60 wakati ambao chama hicho kimekuwa kinara wa
Utawala bora na Demokrasia kwa wananchi wa makundi yote.
Aidha, aliwataka viongozi na
watendaji wa Chama na Jumuiya zake kuanzia ngazi za Matawi kutekeleza
kwa vitendo agizo la CCM katika kuadhimisha miaka 40 ya kuzaliwa kwa
taasisi hiyo kwa mtindo wa kufanya shughuli za maendeleo na ujenzi wa
taifa kwa kipindi cha mwaka mzima.
“ Nahitaji kuona ofisi zetu
kuanzia ngazi za Matawi hadi Mikoa kunafanyika shughul za ujenzi wa
taifa zinazoashiria kuzaliwa kwa Chama chetu, na kufanya shughuli za
maendeleo katika Sekta mbali mbali kijamii zikiwemo vituo vya watoto
yatima, Nyumba za kulelea Wazee, Vituo vya Afya na Mahospitalini Unguja
na Pemba.”, alisisitiza Naibu Katibu Mkuu huyo wa CCM Zanzibar.
Aliwapongeza Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein pamoja na Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pembe Magufuli kwa juhudi
zao za kusimamia kwa uadilifu fursa za kimaendeleo kwa maslahi ya nchi.
Pia alikiri kuthamini juhudi
zinazofanywa na uongozi wa Chama wa Wilaya hiyo kwa Kusimamia vizuri
utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010/2020, na kuwaagiza
waendelee kuratibu na kufuatilia kwa karibu shughuli zinazofanywa na
Wawakilishi, Wabunge na Madiwani ndani ya Wilaya hiyo.
Akisoma taarifa ya utekelezaji wa
shughuli za Kisiasa ndani ya Wilaya hiyo, Katibu wa CCM Wilaya ya Kati
Unguja, Ali Yussuf alisema viongozi wa wilaya hiyo kwa kushirikiana na
makada wa Chama wametekeleza shughuli za ujenzi wa taifa zikiwemo
kufanya usafi na mikutano ya ndani ikiwa ni moja ya shamrashamra za
kuzaliwa kwa CCM.
Katibu huyo alifafanua kuwa
Wilaya hiyo imejipanga kikamilifu katika kukabiliana na chaguzi za
Kichama na jumuiya kwa lengo la kupatikana viongozi makini na wenye
sifa za kuvusha salama jahazi la CCM katika uwanja wa kisiasa.
Hata hivyo amesema wanaendelea na
ziara maalum kunzia ngazi za mashina hadi Wilaya kwa lengo la kukagua
hali ya kisiasa na kuratibu changamoto zinazowakabili wananchi wa maeneo
mbali mbali ili zitafutiwe ufumbuzi wa kudumu kupitia mamlaka husika.
|
February 7, 2017
CCM Z’BAR YAWATAKA WAFUASI WAKE KUTANGULIZA MBELE DHANA YA UZALENDO.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment