Jeshi
la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, linamshikilia Mbunge wa
Singida Mashariki ambaye pia ni mwanasheria wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu kwa madai ya kutoa kauli za uchochezi.
Akizungumza
na waandishi wa habari ofisini kwake Dar es Salaam jana, Kamanda wa
Kanda Maalumu, Kamishna Simon Sirro, alisema Lissu alikamatwa juzi mjini
Dodoma wakati alipokuwa akitoka katika vikao vya Bunge.
Alisema
baada ya kumkamata, walilazimika kumsafirisha hadi Dar es Salaam ambako
inadaiwa ndiko alikotolea kauli hizo ambazo wanadai zinaweza
kuhatarisha amani ya nchi.
“Tumemkamata
Tundu Lissu juzi mjini Dodoma na kusafirishwa usiku hadi Dar es Salaam
ili aweze kufikishwa kituoni kwa ajili ya kuhojiwa kutokana na kutoa
kauli zake za kichochezi ambazo zinaweza kuhatarisha amani ya nchi,” alisema Sirro.
Alisema
si mara ya kwanza kwa kiongozi huyo kutoa kauli hizo na kuitwa kituoni
kwa ajili ya kuhojiwa, lakini kinachofanyika baada ya kuruhusiwa amekuwa
akiendelea kuzitoa tena.
Sirro
alisema kutokana na hali hiyo, jeshi hilo linaendelea na mahojiano na
kwamba uchunguzi utakapokamilika watamfikisha mahakamani kwa hatua
zaidi.
Alisema
kutokana na hali hiyo, kesho (leo) atatoa taarifa kamili kuhusu
matamshi hayo yanayodaiwa ya kichochezi ili wananchi waweze kujua.
Naye
Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, amesema
anasikitishwa na vitendo vya kukamatwa wabunge wakiwa ndani ya vikao,
huku Ofisi ya Bunge ikikaa kimya bila kutoa tamko.
Akizungumza
jana baada ya kumtembelea Lissu, ambaye yuko mahabusu ya Kituo Kikuu
cha Polisi, Dar es Salaam, Mbowe alisema Ofisi ya Bunge inajua wabunge
wana kinga ya kisheria, lakini wamekuwa hawachukui hatua wala kutoa
kauli yoyote.
“Tunasikitishwa
na vitendo vya kukamata wabunge wakiwa ndani ya vikao vya Bunge na hasa
wabunge wa upinzani, wanaendelea kukamatwa wengine wanafungwa na
wengine wanapotezewa muda wao wa Bunge.
“Wabunge
wanakamatwa Dodoma wanasafirishwa usiku wa manane kama vibaka halafu
wananyimwa dhamana, viongozi wa Bunge hawatoi kauli yoyote… haya mambo
yanayotokea si ya kawaida,” alisema Mbowe.
Alisema Lissu amehojiwa kwa kauli zake zinazodaiwa kuwa za uchochezi, wakati akijadili suala la njaa katika Taifa.
“Sasa
Lissu kama viongozi wengine wa Chadema, vyama vingine vya siasa na
madhehebu mbalimbali ya dini, walitahadharisha hali ya kuwapo kwa njaa
katika Taifa. Lakini ndani ya Bunge kauli ya Serikali iliyotolewa na
Waziri wa Kilimo ilithibitisha kwamba watu zaidi ya milioni 1.5
wanakabiliwa na njaa na karibu 200,000 wana shida kali ya njaa.
“Kauli
alizoongea Lissu zimeshathibitika si za uongo na tunashangaa mwezi
mmoja umepita na Serikali imeshatoa kauli ya kuthibitisha shutuma
zilizotolewa na viongozi wa dini, kisiasa na hata wa kijamii, lakini
bado wamemshika Lissu na wamekataa kumpa dhamana,” alisema.
Mbowe alisema viongozi wa chama hicho watakutana na wanasheria wao kutafakari kwa kina hatua za kuchukua.
“Wamesema
hawawezi kutoa dhamana katika hatua ya sasa, jalada lake litapelekwa
kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) na ndiye atakayetoa maamuzi kuhusiana
na kesi yenyewe. Tumeelekezwa tufuatilie dhamana yake kesho (leo),” alisema.
|
February 8, 2017
JANA TUNDU LISSU KALALA SERO BAADA YA KUNYIMWA DHAMANA...MBOWE ALAANI
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment