Askofu
Mkuu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, amemuomba Rais
John Magufuli kuingilia kati sakata la kutangaza na kushikiliwa Kituo
Kikuu cha Polisi Dar es Salaam watu wanaotuhumiwa kujihusisha na dawa za
kulevya.
Pia
alieleza kushangazwa kwake na baadhi ya wawekezaji na wafanyabiashara
wakubwa nchini kuingizwa katika sakata hilo hata kabla uchunguzi
kufanyika.
Gwajima
ambaye alikuwa ameshikiliwa Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam
alikokwenda baada ya kutangazwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul
Makonda, akituhumiwa kujihusisha na dawa za kulevya, alisema hana mpango
wa kumshtaki mkuu huyo wa mkoa.
Askofu
Gwajima alisema badala yake anakata rufaa kwa Rais Magufuli akimtaka
kufuatilia tuhuma hizo kwa undani kwa watu wanaoendelea kushikiliwa na
Jeshi la Polisi ili waweze kupata haki.
Akizungumza
kanisani kwake Dar es Salaam jana, Gwajima alisema alishikiliwa na
Jeshi la Polisi Mkoa wa Dar es Salaam baada ya kwenda kuitikia mwito
uliotolewa na Makonda kwa ajili ya kutoa ushirikiano kuhusu tuhuma za
dawa za kulevya
Alisema
baada ya kufika kituoni hapo na kufanyiwa mahojiano alikutana na
mfanyabishara na Diwani wa Mbagala Kuu, Yusuph Manji ambaye naye alikuwa
amefika kituoni hapo kwa ajili ya kuitika mwito huo wa Makonda.
"Kwenye
chumba changu tulikuwa mimi na Yusuph Manji, huyu ana kampuni zaidi ya
23 ameajiri Watanzania zaidi ya 5,000, sasa mtu kama huyo
imeshindikanaje kumuita kwa kumpelekea hati ya kuitwa kuhojiwa, badala
yake anatangazwa?"
"Imeshindikanaje
mtu kama Manji kumuita kwa kumuandikia barua ili aende ahojiwe na
ikigundulika achukuliwe hatua, kwa nini atangazwe kabla ya kuchukuliwa
hatua? Ilipaswa aandikiwe barua ya wito kisha uchunguzi ufanyike na
kama akibainika ndiyo achukuliwe hatua, ila kwa sababu mkuu wa mkoa
hakuwa na nia nzuri hata kwa Manji ndiyo maana hakufanya hivyo," alisema Gwajima.
Alisema
hadi alipoachiwa katika kituo hicho bado Manji alikuwa ameshikiliwa na
Jeshi la Polisi, ambapo alihoji sababu ya Manji na wengine wanaoendelea
kushikiliwa kituoni hapo kutofanyiwa uchunguzi na ukaguzi kama
aliofanyiwa yeye ili waachiwe kama yeye au kuchukuliwa hatua kama
wakibainika kujihusisha na biashara hiyo.
"Sioni
sababu ya kuendelea kuwashikilia watu wale bila kuchukuliwa hatua. Kama
mimi nilituhumiwa tena kwa kutangazwa lakini mwishowe ikabainika hakuna
ukweli, nitaamini vipi kama wale waliobaki ndani mikononi mwa Polisi
nao wanahusika?"Alihoji Gwajima.
Gwajima
alisema mbali na Manji na wafanyabishara wengine waliotajwa kuhusika na
biashara hiyo, wamo pia askari wa Polisi ambao nao wanatuhumiwa
kujihusisha na biashara hiyo na wameendelea kushikiliwa kwa amri ya mkuu
wa mkoa.
Kutokana
na hali hiyo, Gwajima alisema ameamua kukata rufaa kwa Rais ili aweze
kuwaangalia watu hao kwa jicho la tatu na tuhuma dhidi yao ziweze
kuchunguzwa na ukweli ujulikane.
"Mheshimiwa
Rais ninakuomba sana, kuna wale watu wengine ambao nilikuwa nao, ambao
ni wafanyabishara na walitangazwa kama mimi, naomba uwatazame kwa macho
ya huruma ili tuhuma zao zishughulikiwe, kuliko kuendelea kukaa kwenye
giza chini mule, kwa niaba yao ninakata rufaa kwako naomba uwahurumie.
"Kuna
askari Polisi wapo ndani kwa wiki ya pili sasa kwa amri ya Makonda,
mimi naomba niwasemee leo, kama mimi imeonekana kuwa sina makosa, vipi
kuhusu wao? Nampongeza mheshimiwa Rais kwa kuingia katika vita ya dawa
za kulevya naomba atazame jambo hili, "alisisitiza Askofu Gwajima.
Alisema
kuwa alichogundua ni kuwa Rais anahitaji msaada wake hivyo anaingia
katika kazi ya kumsaidia Rais kwa maelezo kuwa inawezekana anapata
taarifa zisizo za ukweli.
Gwajima
alisema kuwa leo amepanga kwenda Kituo Kikuu cha Polisi kwa ajili ya
kuwaona watuhumiwa wengine ambao wanaendelea kushikiliwa.
Aeleza alivyokaguliwa
Katika
hatua nyingine, Gwajima alisimulia waumini wa kanisa lake namna
shughuli ya ukaguzi dhidi yake ilivyoendeshwa na Jeshi la Polisi, huku
akidai amechiwa baada ya kubainika tuhuma dhidi yake hazikuwa na ukweli.
Alisema
baada ya kuhojiwa alielezwa anatakiwa kwenda kwa Mkemia Mkuu wa
Serikali kwa ajili ya kufanyiwa vipimo ili kubaini kama anajihusisha na
utumiaji wa dawa za kulevya ama la, ikiwa ni pamoja na kufanyiwa
upekuzi nyumbani kwake ambapo alieleza kuwa licha ya kufanyiwa yote hayo
Polisi walifikia pia hatua ya kukagua akaunti zake za fedha.
"Kwa
sababu mimi tangu kuzaliwa sijawahi kuonja mambo hayo, lakini
walivyopima wakakuta hamna chochote na wakanipa fomu kuonesha hawajakuta
kitu.
"Niliwaambia
kwangu mkikuta hata kipisi cha sigara andikeni dawa za kulevya,
tulifika kwangu nyumba yangu ina ghorofa tatu wakakagua zote na
hawakukuta kitu walichotaka," alisema
Aliongeza kuwa,"wakaona
haitoshi, wakahamia kwenye akaunti zangu za benki na mimi nikawaruhusu
waendelee walipofanya uchunguzi wao wakabaini hakuna kitu cha kuweza
kunikamatia, hawakupata kitu wakaamua kuniachia,".
Gwajima alisema hana mpango wa kumshtaki Makonda ama kumfungulia kesi bali anajua cha kumfanya.
|
February 13, 2017
MASAA 72 YA ASKOFU GWAJIMA MAHABUSU YA POLISI
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment