Na: Lilian Lundo – MAELEZO – Dodoma
Mfuko wa Maendeleo ya Vijana
umetoa mikopo yenye jumla ya Shilingi 1,867,896,520 kwa vikundi vya
vijana 309 katika Halmashauri 94.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri
Mkuu, Kazi Vijana Ajira na Watu Wenye Ulemavu Anthony Mavunde ameyasema
hayo leo Bungeni, Mjini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa
Viti Maalum Zainab Katimba alipotaka kujua idadi ya vijana walionufaika
kupitia mfuko huo na namna ambavyo mikopo hiyo imebadilisha maisha yao.
“Lengo la kuanzishwa kwa mfuko wa
Maendeleo ya Vijana ni kuwawezesha vijana wote nchini (Tanzania Bara)
kupata mitaji kwa njia ya mikopo yenye masharti nafuu ili kuanzisha au
kuendeleza miradi yao ya uzalishaji mali,” alifafanua Mavunde.
Aliendelea kwa kusema kuwa fedha
za mikopo zitokanazo na Mfuko huo umekuwa msingi mzuri katika kuwaandaa
vijana kujiajiri na kuajiri vijana wengine na hata kukuza vipato vyao.
Mavunde alitaja shughuli ambazo
vijana hao wamekuwa wakishiriki mara wanapopata mikopo hiyo kuwa ni
uanzishwaji wa viwanda vidogo vidogo, kilimo, ufugaji pamoja usindikaji
wa mazao.
Aidha amesema kuwa shughuli hizo
zimewafanya vijana kuachana na utegemezi na badala yake kutumia muda wao
mwingi katika kuzalisha na hivyo kuongeza tija katika uchumi wa Nchi.
Vile vile amesema kwamba, vipo
vikundi ambavyo kupitia mfuko huo vimekuwa kielelezo cha dhati katika
kubadili mtizamo wa vijana wa kutegemea kuajiriwa hadi kujiajiri
wenyewe na kukuza vipato vyao.
Alivitaja vikundi hivyo kuwa ni
kikundi cha Thyroid Group kutokana Halmashauri ya Chunya ambacho
kinasambaza Taa za Solar Vijijini, kikundi cha Miranaco Group ambacho
kinamiliki duka kubwa la dawa za Binadamu kutoka Halmashauri ya Mbozi,
kikundi cha Maswa Family kinachoshughulika kutengeneza chaki na Meatu
Milk kinachotengeneza maziwa kutoka mkoani Simiyu.
Aidha, ili kuboresha mfuko huo
Serikali imekuwa ikifanya ufuatiliaji na tathmini za mara kwa mara kwa
lengo la kuhakikisha ufanisi unakuwepo na kubaini changamoto za
kiutendaji zinazojitokeza.
Hata hivyo, katika mwaka huu wa
fedha Serikali inapitia upya mwongozo wa utoaji fedha kupitia mfuko huo
wa Maendeleo ya Vijana ambao ulioanzishwa mwaka 2013 ili kuwawezesha
vijana wengi kuanzisha viwandaa vidogo vidogo katika kuendana na Sera ya
Nchi ya kwenda kwenye Uchumi wa Viwanda.
|
February 6, 2017
MFUKO WA MAENDELEO YA VIJANA YATOA MIKOPO KWA ZAIDI YA VIKUNDI 309
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment