Katika kuhakikisha kuwa biashara
haramu ya dawa za kulevya inakomeshwa hapa nchini na kwa kuzingatia
dhamira ya serikali ya awamu ya tano ya kupambana na tatizo la dawa za
kulevya, Jeshi la Polisi nchini limetoa maelekezo kwa Makamanda wa
Polisi katika mikoa yote kuongeza nguvu za Oparesheni katika mapambano
dhidi ya biashara haramu ya dawa za kulevya kwa kuwakamata wanaotumia,
wanaouza na wanaosafirisha.
Aidha, Jeshi la Polisi nchini
limewaagiza Makamanda wote pindi wanapoendesha oparesheni dhidi ya dawa
za kulevya kutokuangalia sura ya mtu, cheo, wadhifa wala nafasi
aliyonayo katika jamii.
Katika hatua nyingine, Jeshi la
Polisi nchini linakemea vikali tabia ya baadhi ya wananchi
wanaokusanyika katika vituo vya Polisi pindi baadhi ya watuhumiwa wa
makosa mbalimbali wanapotakiwa kufika kwenye vituo hivyo kwa ajili ya
kuhojiwa kuhusiana na tuhuma wanazokabiliwa nazo. Ni marufuku kwa mtu
ama kikundi chochote kukusanyika katika kituo cha Polisi bila ya kuwa na
sababu ya msingi na watakaobainika watashughulikiwa kwa mujibu wa
sheria.
Jeshi la Polisi nchini, linatoa
wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu
zikiwemo za watu wanaojihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya na
taarifa hizo zitafanyiwa kazi kwa siri ili kuhakikisha nchi inaendelea
kuwa katika hali ya usalama.
Imetolewa na:
Advera John Bulimba-ACP,
Msemaji wa Jeshi la Polisi,
MAKAO MAKUU YA POLISI.
|
February 14, 2017
POLISI YAAGIZA MAKAMANDA WAKE KUONGEZA NGUVU MAPAMBANO YA DAWA ZA KULEVYA
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment