Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli,
ameviagiza vyombo vyote vya ulinzi na usalama kuongeza nguvu katika
mapambano dhidi ya dawa za kulevya kwa kuhakikisha vinasimamia sheria
ipasavyo ili kukabiliana na tatizo hilo hapa nchini.
Mhe.
Rais Magufuli ametoa agizo hilo leo tarehe 12 Februari, 2017 Ikulu
Jijini Dar es Salaam, muda mfupi baada ya kuwaapisha Kamishna Mkuu wa
Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya Bw. Rogers William
Siyanga, Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt. Anna Peter Makakala, Balozi
wa Tanzania nchini Ubelgiji Mhe. Joseph Edward Sokoine, Balozi wa
Tanzania nchini Algeria Mhe. Omar Yusuf Mzee na Balozi wa Tanzania
nchini Uganda Mhe. Grace Aaron Mgovano.
Mhe.
Dkt. Magufuli amewataka viongozi wote wa Serikali kuungana na vyombo
vya dola katika mapambano dhidi ya watu wanaojihusisha na biashara
haramu ya dawa za kulevya na ametaka mapambano hayo yasifanywe kwa mzaha
wala kwa kuangalia majina ya watu, vyeo vyao na taasisi wanazoongoza.
Mhe.
Rais Magufuli amewapongeza viongozi wote wa mikoa walioanza kukamata
watu wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya na amewaomba
Watanzania wote waunge mkono juhudi za kukabiliana na wanaofanya
biashara na kutumia dawa za kulevya ambazo zinazidi kuangamiza nguvukazi
ya Taifa.
“Niwaombe
ndugu zangu tuungane katika vita hii dhidi ya dawa za kulevya,
waandishi wa habari na wana mitandao tuweke mbele Utanzania wetu,
akitokea mtu anapambana na dawa za kulevya tumuunge mkono badala ya
kumchafua.
“Vita
hii ni kubwa hatuwezi kwenda nayo kwa mzaha na Serikali itahakikisha
inasimamia sheria namba 5 ya mwaka 2015 iliyohusu kuzuia na kupambana na
dawa za kulevya ambayo ilitungwa na Bunge la 10 lililoongozwa na Spika
Anna Makinda na sheria hiyo ikatiwa saini na Rais Mstaafu wa Awamu ya
Nne Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, nawapongeza sana kwa kutunga sheria
hii.” Amesisitiza Mhe. Rais Magufuli
Pia,
Mhe. Dkt. Magufuli amesema takwimu zinaonesha kuna watanzania 1,007
wamekamatwa na kufungwa gerezani katika nchi mbalimbali baada ya
kupatikana na makosa ya kujihusisha na dawa za kulevya, na amemuagiza
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Mabalozi
wote wanaoiwakilisha Tanzania katika nchi hizo kutojihusisha kuwatetea
waliofungwa kwa makosa hayo na badala yake waache sheria za nchi husika
zichukue mkondo wake.
Wakati
huo huo, Mhe. Rais Magufuli amemtaka Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Dkt.
Anna Peter Makakala kufanya mabadiliko makubwa ndani ya Idara ya
Uhamiaji nchini kutokana na utendaji wake kutoridhisha.
“Nataka
ukafanye mabadiliko makubwa (Total Reform), nataka Uhamiaji izalishe
fedha kwa ajili ya nchi hii, nataka ukadhibiti utoaji hati za kusafiria
(Passports) maana zimekuwa zikitolewa hovyohovyo” amesisitiza Mhe. Rais
Magufuli.
Hafla
ya kuapishwa kwa viongozi hao pamoja na kula kiapo cha uadilifu kwa
viongozi wa umma kilichoongozwa na Kamishna wa Maadili Mhe. Jaji Mstaafu
Harold Nsekela, imehudhuriwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu
Hassan, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, Kaimu Jaji Mkuu Mhe. Prof.
Ibrahim Juma, Mawaziri, Makatibu Wakuu wa Wizara mbalimbali na Wakuu wa
vyombo vya Ulinzi na Usalama.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
12 Februari, 2017
No comments:
Post a Comment