Jacquiline Mrisho na Eliphace Marwa – MAELEZO.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli
amemkabidhi Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa kazi ya kuzuia na
kupambana na dawa za kulevya akiwa kama Mwenyekiti wa Tume ya Kudhibiti
Dawa hizo nchini.
Rais
Magufuli ameyasema hayo leo Ikulu Jijini Dar es Salaam wakati
akiwaapisha Kamishna Jenerali wa Jeshi la Uhamiaji, Anna Peter Makakala,
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya,
Rogers William Sianga pamoja na mabalozi watatu Mhe. Omary Yusuph Mzee,
Mhe.Joseph Edward Sokoine pamoja na Mhe. Grace Aron Mgovano aliowateua
hivi karibuni.
Dkt.
Magufuli amesema kuwa Waziri Mkuu anatajwa kwenye Sheria Na.5 ya mwaka
2015 kuwa ni Mwenyekiti wa Tume hiyo ambapo Wajumbe wake ni Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Waziri wa Mambo ya Ndani, Waziri wa
Elimu ana Mafunzo ya Ufundi, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo, Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Waziri wa
Fedha na Mipango, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto pamoja na Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
“Nalipongeza
sana Bunge la kipindi cha mwaka 2010 – 2015 chini ya Spika mstaafu,
Mhe. Anne Makinda lililopitisha Sheria hii baada ya kuona sheria za
mwanzo za kupambana na dawa za kulevya hazina nguvu hivyo Wabunge wa
wakati ule walisimama kwa pamoja bila kujali itikadi za vyama vyao
wakapitisha sheria hii,” alisema Dkt. Magufuli.
Aidha,
Dkt. Magufuli amempongeza Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Kikwete kwa kusaini
sheria hiyo haraka mara baada ya Bunge hilo kuipitisha kwa sababu alijua
madhara ya dawa za kulevya katika nchi yetu.
Amefafanua
kuwa sheria imeeleza wazi katika kifungu cha 10 cha Sheria Na.5 ya
mwaka 2015 kuwa jukumu la kupambana na dawa za kulevya linasimamiwa na
Serikali pekee yaani Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais wa
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Makamo wa Rais, Waziri Mkuu,
Mawaziri, Wakuu wa Mikoa na Wilaya pamoja na Wakurugenzi wa Halmashauri
za Wilaya au mtu yoyote atakayekuwa amepewa mamlaka ya kusimamia
Serikali.
Kwa
upande wake Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa amesema kuwa Taifa
limeendelea kushuhudia kizazi chetu kikiendelea kudidimia kwa sababu ya
matumizi ya dawa za kulevya na Serikali kwa mipango yake imeendelea
kukemea, kudhibiti na kuchukua hatua mbalimbali dhidi ya wazalishaji,
wasambazaji, wauzaji na watumiaji wa dawa hizo.
“Jambo
hili limeleta athari kubwa sana kwani vijana wetu wengi wamepoteza
uwezo wa kujisimamia katika shughuli zao za maendeleo kwa sababu baada
ya matumizi tumeona athari kadhaa zikiwezo za kudhoofishwa kwa mwili,
uwezo wa kutafakari pamoja na kutoweka kwa uwezo wa kufanya
kazi,”alisema Waziri Mkuu Majaliwa.
Waziri
Mkuu Majaliwa ameongeza kuwa Taifa hili la Watanzania kwa kiasi kikubwa
linawategemea vijana waweze kuleta msukumo wa maendeleo ndani ya nchi
hivyo jambo hili likiachiwa linaweza kuleta athari kubwa katika ukuaji
wa uchumi na maendeleo yetu kwa ujumla wake.
Alisisitiza
kuwa vita hii ilianza, inaendelea na itaendelea kupiganwa hadi
imalizike hivyo Watanzania hawana budi kuunga mkono jitihada zozote
zinazofanywa na Serikali kuhakikisha wanatokomeza uzalishaji,
usambazaji, uuzaji na matumizi yake kwa namna yoyote ile, kila mmoja
anatakiwa kushiriki kikamilifu ili kubaini matumizi ya dawa za kulevya
ndani ya nchi hii.
No comments:
Post a Comment