Mkuu
wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema hawezi kufika mbele ya
Kamati ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge kuhojiwa kwa kuwa hajapokea
barua ya kuitwa.
Makonda jana alisema hatoweza kwenda mbele ya kamati hiyo bila barua rasmi iliyomtaka kufanya hivyo.
Bunge
lililokuwa likiendelea na vikao vyake Dodoma kabla ya kuahirishwa juzi,
lilipitisha uamuzi wa kuwataka Makonda na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru,
Alaxander Mnyeti, kufika mbele ya kamati hiyo na kuhojiwa kutokana na
kauli walizozitoa, zinazodaiwa kuudharau mhimili huo wa dola.
Lakini Makonda alisema jana “hilo suala la mimi kuitwa kwenye kamati nalisikia na kulisoma kwenye magazeti."
"Sina uhakika ni lini wamefikia uamuzi huu wa kuniita na hata kama wamefikia uamuzi huo, sijaletewa barua rasmi.”
Baada
ya Bunge kupitisha uamuzi huo wa kuitaka Ofisi ya Bunge iwaandikie
barua viongozi hao, juzi baadhi ya wabunge walihoji kauli ya Katibu wa
Bunge, Dk. Thomas Kashililah, kwamba azimio la chombo hicho cha kutunga
sheria kumtaka Makonda kufika mbele ya kamati kujieleza kuhusu tuhuma za
kuudharau mhimili huo, halikufuata utaratibu.
Hatua
hiyo iliamsha hasira kwa baadhi ya Wabunge na kuomba mwongozo kuhoji
kwa nini Katibu wa Bunge ametoa kauli ambayo inakinzana na makubaliano
ya Bunge.
Mbunge
wa Ukonga, Mwita Waitara na mwezake wa Iringa Mjini Mchungaji Peter
Msigwa (wote Chadema) walihoji kuhusu kauli ya Dk. Kashililah.
Waitara alisema, “Asubuhi
ya leo ( juzi) nimetumiwa ‘clip’ ya sauti ya Katibu wa Bunge akikosoa
uamuzi wetu hapa na pia gazeti la Habari Leo, Ukurasa wa 25, kuna habari
imeandikwa.
"Katika taarifa hii, Katibu wa Bunge anasema maazimio ya Bunge yalikosewa na hayakufuata utaratibu,” alisema na kuongeza kuwa: “ Kwa maana nyingine, hatatekeleza kile tulichokubaliana.”
Mchungaji
Msigwa wakati akichangia taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo
ya Nje, Ulinzi na Usalama, alieleza kuwa hajafurahishwa na kauli ya
Katibu wa Bunge.
Alisema
Katibu wa Bunge amekosea kwenda katika vyombo vya habari na kudai
chombo hicho cha kutunga sheria kimekosea kwa kuwa anafanya kazi ya
Bunge na kwamba hajaajiri wabunge na anapaswa kufuata maagizo yao.
Hoja
ya kutaka kina Makonda washughulikiwe iliwasilishwa na Mbunge wa
Ukonga, Mwita Waitara (Chadema) katikati ya wiki na ilijadiliwa na
kuungwa mkono na wabunge wote, wakiwamo mawaziri kwa kusema ‘ndiyo’.
Akiwasilisha
hoja hiyo kipindi cha usiku baada ya kipindi cha asubuhi kutoruhusiwa
na Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge, Waitara alisema: “Haya mambo
ndiyo yamejirudia wakati nikiangalia televisheni ya Clouds, Makonda
akionekana akisema sisi humu bungeni tunasinzia.”
Alibainisha
kuwa kwa mujibu wa Katiba ibara ya 63 (2), Bunge ndicho chombo kikuu
kwa niaba ya wananchi katika kuisimamia na kuishauri Serikali na
linapitisha bajeti inayotumiwa na wateule hao wa Rais.
Alisema si sawa kwa wakuu wa mikoa na wilaya kuwaweka rumande wabunge, madiwani na watumishi wa serikali.
“Bunge
linaingia katika majaribu makubwa ya kudharauliwa. Tunakula kiapo humu,
tunaamua kwa niaba ya Watanzania, lakini Mkuu wa Wilaya anasema hawa ni
wapuuzi na Mkuu wa Mkoa anasema hawa wanalala tu.”
Baada
ya hoja hiyo, Waitara alitaka ijadiliwe na Bunge na kutoa maazimio ili
kurejesha heshima ya chombo hicho, hoja ambayo Chenge aliipokea na kutoa
nafasi kwa wabunge wanne kujadili kutokana na muda kuwa mfupi.
Mbunge wa Ulyankulu (CCM), John Kadutu, alisema: “Nimehuzunika
sana wabunge tunafika mahali tunadharauliwa, halafu watu tunaangalia
tu. Haya ambayo yametokea kwa Makonda na Arumeru, pia yametokea Manispaa
ya Dodoma.Mkurugenzi anaongea na wabunge kama watoto.
“Nadhani
hata ile sheria ya Marekani wenzetu wanaoteuliwa kwa ngazi za juu
lazima wapelekwe bungeni hapa kwetu ingefaa kuletwa ili watu wa aina hii
tuweze kuwamaliza hapa hapa.
"Wapo wanaodhani wako juu yetu.”
Alisema ni jambo la hatari kujenga serikali yenye kiburi na kusisitiza “unapotaka
kutoa pepo halibembelezwi. Unataka kupunga majini huwezi
kubembeleza.Lazima ukazane kupunga jini litoke. Hatuwezi kutoa pepo kwa
lugha nyepesi nyepesi (akipunguza sauti) pepo toka, haiwezekani. Kama ni
pepo tulikemee litoke.”
Ester
Bulaya (Bunda Mjini–Chadema) alieleza Makonda alivyompigia simu na
kutamba kushughulikia wabunge kwa kuwa yuko karibu na ‘Bwana mkubwa’,
huku akisisitiza kuwa Mkuu huyo wa Mkoa hakutengenezwa kuwa kiongozi.
“Makonda alinipigia simu na kunitisha kwamba yeye yuko karibu na Bwana mkubwa, atatushughulikia wabunge.
Alisema
ataanza na (Joseph Kasheku) Msukuma (Geita-CCM), Halima Mdee
(Kawe-Chadema), Esther Matiko (Tarime Mjini-Chadema), Sugu (Joseph
Mbilinyi-Chadema Mbeya Mjini) na (Mchungaji Peter) Msigwa (Iringa
Mjini-Chadema),” alisema.
Mbunge wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea alisema “Ni
lazima heshima ya Bunge ilindwe kwa gharama yoyote. Makonda anawapigia
simu wabunge akitaja mmoja wa mawaziri kuwa ndiye anatuma wabunge
wamtukane.”
Naye
Msukuma alisema haiwezekani Makonda afanye kazi ya polisi na kuhoji
aliko Mkuu wa Jeshi la Polisi, makamanda na makamishna wake.
“Makonda
ni nani katika hii nchi? Kama (David) Jairo (aliyekuwa Katibu Mkuu wa
Wizara ya Nishati na Madini) alitoka kwa azimio la Bunge, Makonda ni
nani? Mimi niko tayari kupambana na Makonda,” alisema Msukuma.
Hoja
hiyo pia ilitolewa ufafanuzi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George
Masaju na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge,
Kazi, Vijana na Watu wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, wakitaka wahusika
hao wasikilizwe kwanza na kuachia ngazi zingine iwapo watabainika
kutenda kosa.
Baada
ya wabunge kuchangia, Chenge alitoa nafasi kwa Waitara ambaye
alihitimisha hoja hiyo na kutoa maazimio manne ambayo Mwenyekiti huyo wa
Bunge aliyafafanua na kupitishwa.
Maazimio
hayo ni pamoja na Makonda na Mnyeti kuitwa mbele ya Kamati ya Haki,
Kinga na Madaraka ya Bunge ili kuhojiwa juu ya kauli zao zenye mwonekano
wa udhalilishaji kwa Bunge, ambalo ni mhimili pacha na ule wa utawala
wanaoutumikia.
No comments:
Post a Comment