Serikali imesema kuwa katika
kudhibiti matumizi holela ya fedha za kigeni, Benki Kuu kwa kushirikiana
na Mamlaka ya Mapato Tanzania imeongeza usimamizi katika maduka ya
kubadilishia fedha za kigeni ambapo taarifa za kila muamala wa fedha za
kigeni unaofanywa zinapaswa kuoneshwa.
Kauli hiyo imetolewa Bungeni leo
na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt Ashatu Kijaji, wakati
akijibu maswali ya Mbunge wa Igunga Mhe. Dalaly Peter Kafumu aliyetaka
kupewa ufafanuzi juu ya Kwanini Serikali isidhibiti matumizi holela ya
dola nchini ili kupunguza utakasishaji wa fedha na kuimarisha ukuaji wa
uchumi kama zinavyofanywa nchi nyingi duniani.
Aidha, Dkt Kijaji alifafanua
hatua zimechukuliwa pia kuhakikisha kuwa miamala ya fedha za kigeni
inayofanywa na mabenki ni ile inayohusu shughuli za kiuchumi tu ili
kulinda thamani ya shilingi.
Vilevile, tamko na mwongozo
uliotolewa na Serikali mwaka 2007, ulieleza kuwa bidhaa na huduma
zinazowalenga watalii au wateja wasio wakazi wa Tanzania, bei zake
zinaweza kunukuliwa kwa sarafu mbili, yaani shilingi ya kitanzania na
sarafu ya kigeni na malipo kufanyika kwa sarafu ambayo mlipaji atakuwa
nayo. Pia, mkazi yeyote wa Tanzania asilazimishwe kulipia bidhaa au
huduma yoyote hapa nchini kwa fedha za kigeni.
“Msingi wa kuruhusu soko huru la
fedha za kigeni hapa nchini ni hatua ya makusudi ambayo ilichukuliwa na
Serikali ili kuiwezesha nchi kuondokana na hali ya kuadimika kwa fedha
za kigeni ilikuwa dola za Kimarekani milioni 4,093.7 wakati amana za
fedha za kigeni za wakazi wa Tanzania zilikuwa dola za Kimarekani
milioni 2,933.1 na rasilimali za fedha za kigeni za mabenki zilikuwa
kiasi cha dola za Kimarekani milioni 1,021.1” alisema Dkt. Kijaji.
Dkt Kijaji ameeleza kuwa
Tanzania ina urari wa biashara ya nje ambao umetokana na sera huru za
kigeni, ambazo zimechangia kuimarisha uchumi kwa zaidi ya miaka 10
iliyopita, wastani wa ukuaji wa uchumi wa Taifa letu katika kipindi cha
miaka kumi iliyopita ulikua ni asilimia 7, ikiwa ni wastani wa juu sana
ikilinganishwa na nchi nyingine duniani.
“Mfano, wastani wa ukuaji wa
uchumi wa nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara ni asilimia 5.4 katika
kipindi hicho wakati ule wa nchi zinazoibukia kiuchumi ulikua ni
asilimia 5.8” alisisitiza Dkt. Kijaji
Alisema kuwa njia zinazotumika
kutakatisha fedha ni pamoja na kuziingiza haramu kwenye taasisi za fedha
na kuziwekeza katika rasilimali halali kama ardhi na nyumba. Baadhi ya
mambo yanayowapatia wahalifu fedha haramu ni pamoja na biashara ya dawa
za kulevya, rushwa, ujangili, ujambazi, ukwepaji kodi n.k. Aidha fedha
zinazotokatana na shughuli za kihalifu zinaweza kuwa shilingi za
Kitanzania, dola za Kimarekani au fedha nyingine yoyote ile.
Naibu Waziri huyo wa Fedha na
Mipango amesema ziko kanuni ambazo zinafuatwa na vyombo vya fedha ili
kuzuia utakatishaji wa fedha zote zilizopatikana kutoka vyanzo haramu na
sio dola pekee huku akibainisha kuwa Benki Kuu ya Tanzania ina jukumu
la usimamizi wa taasisi za fedha, hufuatilia mabenki ili kuhakikisha
kuwa kanuni hizo zinafuatwa.
|
February 7, 2017
SERIKALI INAENDELEA KUDHIBITI MATUMIZI HOLELA YA FEDHA ZA KIGENI
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment