KWA MAONI AU USHAURI E-mail: inocomm2014@gmail.com, PIGA SIMU: 0714555668

www.utt-pid.org


TEMBELEA: www.utt-pid.org

February 7, 2017

DK.KAWAMBWA AGHARAMIA MIL.17 KUMALIZA TATIZO LA UMEME S/SEKONDARI KINGANI

Dk.Shukuru
Na Mwamvua Mwinyi,Bagamoyo
MBUNGE wa jimbo la Bagamoyo ,Dk.Shukuru Kawambwa,ametatua kero ya ukosefu wa umeme katika shule ya sekondari ya kingani ,kata ya Kisutu,kwa kugharamia zaidi ya mil.17 hivyo tatizo hilo kwasasa kubakia historia.
Wanafunzi na walimu shuleni hapo ,wameanza kunufaika umeme wa uhakika kutoka Tanesco baada ya kuteseka kwa kipindi kirefu bila kupata huduma hiyo.
Mwalimu mkuu wa shule ya sekondari Kingani,Method Kunambi,aliyasema hayo wakati akizungumza na wazazi wa wanafunzi shuleni hapo,kuhusu maendeleo ya shule na changamoto zinazowakabili.
Alieleza kuwa nishati hiyo ina mchango mkubwa kwa wanafunzi ili waweze kujisomea nyakati yoyote ili kukuza taaluma zao.
Alisema tatizo hilo lilidumu kwa miaka nane tangu waanze kufanya mchakato wa kuomba kupata umeme mwaka 2007.
Kunambi alisema,shirika la umeme Tanesco lilihitaji kiasi cha sh.mil.15,513,811.6 kwa ajili ya transformer,upatikanaji wa umeme ambapo walishindwa kumudu kulipia gharama hizo.
“Mwaka 2014 jitihada zetu ziligonga mwamba na kushindwa kupata wadau kabisa wa kutusaidia,ambapo mbunge alijitokeza kutusaidia kulipia gharama za transformer na service line mi.13.569.845.65 kupitia mradi wa REA “
“Gharama hizo hazikutosha kupata umeme shuleni mwaka 2016 hiyo ,dk.Kawambwa kupitia mfuko wa jimbo alilipia gharama zilizobakia mil.3,458.468 na sasa tumeingiziwa umeme”alisema mwalimu Kunambi.
Hata hivyo Kunambi,alieleza licha ya kumaliza tatizo hilo lakini bado wana tatizo la uhaba wa viti 77 na meza 107 kwa wanafunzi, viti 38 na meza 38 kwa walimu ,nyumba za walimu 59 ,madarasa, maabara na hosteli za wavulana nne.
Akishukuru kwa niaba ya wazazi ,mwenyekiti wa jumuiya ya wazazi Bagamoyo,alhaj Abdul Sharif,alisema mbunge huyo kaonyesha ujali na kuvalia njuga suala hilo muhimu.
Alisema umeme huo utasaidia wanafunzi watasoma kwa vitendo,walinzi wataweza kulinda kwa usalama zaidi na walimu kufanya kazi zao kiufanisi.
Alhaj Sharif ,alisema ni viongozi wachache wa kuchaguliwa ambao wana moyo wa kujitolea fedha zao kwa ajili ya jamii hivyo dk.Kawambwa anastahili pongezi kubwa.
Nae katibu wa mbunge wa jimbo la Bagamoyo,Magreth Masenga akizungumza kwa niaba ya dk.Kawambwa alipokea shukrani zilizotolewa na walimu na wazazi shuleni hapo. Magreth alisema ,mbunge  huyo ataendelea kusimamia kero zinazowakabili wananchi ili kuhakikisha maendeleo ya jimbo yanapiga hatua.

No comments:

Post a Comment