KWA MAONI AU USHAURI E-mail: inocomm2014@gmail.com, PIGA SIMU: 0714555668

www.utt-pid.org


TEMBELEA: www.utt-pid.org

February 6, 2017

VISIWA VYA UKEREWE KUPATA UMEME JUNI 2018

ukele
Kamishna Msaidizi- Nishati Jadidifu kutoka Wizara ya Nishati na Madini Mhandisi Styden Rwebangila, (kushoto) akielezea mafanikio ya sehemu ya nishati jadidifu chini ya   Idara ya Nishati katika upatikanaji wa umeme wa uhakika katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika jijini Dar es Salaam mapema tarehe 06 Februari, 2017. Kulia ni Mtaalam wa Nishati Jadidifu, Emillian Nyanda.
ukele 1
Sehemu ya waandishi wa habari wakifuatilia maelezo yaliyokuwa yanatolewa na Kamishna Msaidizi- Nishati Jadidifu kutoka Wizara ya Nishati na Madini Mhandisi Styden Rwebangila (hayupo pichani)
ukele 2
Kamishna Msaidizi- Nishati Jadidifu kutoka Wizara ya Nishati na Madini Mhandisi Styden Rwebangila, akisisitiza jambo katika mkutano huo.

Na Greyson Mwase, Dar es Salaam
Visiwa vidogo vilivyopo katika Ziwa Viktoria vinatarajiwa kupata umeme wa uhakika ifikapo Juni mwakani.
Hayo  yalielezwa na Kamishna Msaidizi- Nishati Jadidifu kutoka Wizara ya Nishati na Madini Mhandisi Styden Rwebangila, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam wakati alipokuwa akielezea mafanikio yaliyopatikana Sekta ya Nishati kupitia  Nishati Jadidifu chini ya   Idara ya Nishati katika upatikanaji wa umeme wa uhakika.
Alisema kuwa, wakandarasi wameshaanza kuweka miundombinu   kwa ajili ya  umeme wa jua ambapo miradi hiyo inatarajiwa kukamilika kwa asilimia mia moja ifikapo mwezi Juni mwakani.
Akielezea mipango ya Serikali  katika kuhakikisha kuwa nishati ya  umeme inakuwa ni ya uhakika Mhandisi Rwebangila alisema Wizara inahamasisha vyanzo vingine vya uzalishaji wa umeme kama vile jua, upepo, jotoardhi na kuongeza kuwa inakaribisha wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi kutafiti na kutumia  vyanzo hivyo.
Alisema  kwa upande wa jotoardhi utafiti ulifanyika na kuonesha maeneo ya Songwe na Ziwa Ngozi mkoani Mbeya na Mlima Meru mkoani Arusha yana viashiria vya jotoardhi.
Aliongeza kuwa mara baada ya utafiti kukamilika mwishoni mwa mwaka huu, visima vinatarajiwa kuanza kuchimbwa kwa ajili ya uzalishaji wa nishati ya jotoardhi.
Aliendelea kutaja mipango mingine kuwa ni pamoja na  uanzishwaji wa mwongozo   kwa ajili ya mfumo wa umeme kwenye majengo na  wa udhibiti wa matumizi ya umeme viwandani.
Alisema pia, Wizara inatarajia kuanzisha mfumo mpya wa  uhifadhi data na utoaji  taarifa  za Nishati Jadidifu ujulikanao kama  Tanzania  Renewable  Energy Management Information System (TREMIS) utakaowezesha wawekezaji ndani na nje ya nchi  kubaini fursa za uwekezaji zilizopo katika  sekta ya Nishati Jadidifu.
Alisema katika mfumo huo kutawekwa  taarifa mbalimbali kuhusu,  tafiti mbalimbali  na fursa za uwekezaji katika nishati jadidifu , sera, sheria na taratibu ili kuvutia wawekezaji kutoka  ndani na nje ya nchi.
“Kupitia mfumo huu kutakuwa hakuna haja ya mwekezaji kutoka nje ya nchi kufunga safari hadi Tanzania kwa ajili ya kupata  taarifa,  taarifa zote zitakuwepo katika mfumo huu utakaounganishwa na tovuti ya  Wizara,” alisema Mhandisi Rwebangila.

No comments:

Post a Comment