KWA MAONI AU USHAURI E-mail: inocomm2014@gmail.com, PIGA SIMU: 0714555668

www.utt-pid.org


TEMBELEA: www.utt-pid.org

February 14, 2017

WIZARA YA AFYA YATOA TAARIFA KUHUSU SIKU YA KIFAFA DUNIANI TAREHE 13 FEBRUARI. 2017.

tanzania
Siku ya ugonjwa wa kifafa duniani huadhimishwa duniani kote Jumatatu ya pili ya mwezi wa Februari kila mwaka. Kauli mbiu ya siku hii kwa mwaka huu 2017  ni ‘WEKA UGONJWA WA KIFAFA KWENYE TASWIRA’, kwa kiingereza ni ‘PUTTING EPILEPSY IN THE PICTURE’ . Kauli mbiu hii ina lengo la kuhamasisha Jamii kuutambua zaidi ugonjwa huu.
Tanzania ina idadi kubwa ya wagonjwa wa kifafa na katika Afrika na Duniani kwa ujumla, na ni mojawapo kati ya nchi zenye wagonjwa wengi zaidi. Mfano vijiji vya Mahenge idadi ya wagonjwa hawa ni kubwa hadi kufikia wagonjwa 37.5 kwa kila idadi ya watu1000. Hivyo kuna zaidi ya idadi ya watu milioni  moja (1) nchini hapa ambao wana ugonjwa wa kifafa.
Ugonjwa wa kifafa ni moja wapo ya sababu zinazochangia vifo nchini na ugonjwa huu unakadiriwa kuchukua nafasi ya saba (7) hadi nafasi ya kumi na tano (15) kama kisababibishi cha vifo Tanzania. Wagonjwa wa kifafa katika Tanzania wako katika hatari ya kifo mara sita zaidi ukilinganisha na mwananchi wa kawaida kwenye jamii. Zaidi ya 60% ya vifo vinavyotokana na matatizo ya kifafa, husababishwa na athari za ugonjwa wa kifafa moja kwa moja.
Wagonjwa wengi wa kifafa ni vijana, wakiwa na umri wa wastani wa miaka 15. Zaidi ya 24% ya wagonjwa wa kifafa wana ulemavu mwingine wengi wao kutokana na kuangukia moto wakati mgonjwa anapopatwa na degedege.
Mambo mengi yanayosababisha kifafa yanazuilika kuanzia kuumia ubongo wakati mama anapojifungua, magonjwa yanayosababishwa na vijidudu kama ‘parasite’ na ‘bacteria’. Pia katika kipindi cha sasa watu wengi wanaopata ajali za magari , bodaboda na kadhalika hupelekea kuumia kichwani na ubongo kuathirika na hivyo kuugua ugonjwa huu wa kifafa.
Idadi kubwa ya watu nchini wana mtazamo hasi kuhusu kifafa. Zaidi ya 36% ya watu bado wanaamini kuwa ugonjwa  kifafa unatokana na nguvu za giza au kulogwa.
Ugonjwa huu wa kifafa umefanywa kuwa ugonjwa wa siri na zaidi ya 58% ya idadi ya watu huamini unaleta ugonjwa sugu wa akili. Miongoni mwa jamii yetu bado inaaminika ni ugonjwa wa kuambukiza na 50% ya wagonjwa  wa kifafa hupatwa na msongo wa mawazo na kukosa furaha.
Mfano watoto wenye  umri wa kuanza shule wenye tatizo hili la kifafa 45% hawapelekwi shule na 68% ya wanaoenda shule mahudhurio yao  hayaridhishi  na 37%  tu ndio humaliza elimu ya msingi (Primary school education). Watoto hawa hawaruhusiwi kucheza pamoja na wengine hivyo hubakia kufichwa katika jamii.
Zaidi ya 55% ya watu wenye kifafa Tanzania hawana ajira. Watu pia huwakwepa kuwaoa ama kuolewa nao,  na kama wakioa au kuolewa wengi wao huachika ndani ya muda mfupi tu.
Ni asilimia hamsini (50%) tu ya wagonjwa wa kifafa na ndugu zao hutafuta ushauri miezi miwili baada ya dalili za kifafa kuanza. Zaidi ya 70% huenda kuwaona waganga wa jadi na wengine viongozi wa dini. Aidha, ni 60% tu ya wagonjwa wa kifafa hufika kwenye vituo vya afya ndani mwaka mmoja baada ya dalili za kifafa kuanza. Hata hivyo 5-10% ndio huweza kupata matibabu sahihi. Hivyo idadi kubwa ya watu wanaoishi na kifafa Tanzania huendelea kuwa tatizo la ugonjwa huu.
Matibabu ya wagonjwa wenye tatizo hili hutolewa bure kama ilivyo kwenye sera ya Afya ya Taifa kwani ugonjwa huu ni mmoja wapo kati ya magonjwa sugu yaliyoainishwa kwenye sera hii.  Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inagharamia matibabu haya kwa kutoa dawa 3 muhimu katika vituo vya kutolea huduma za afya, dawa hizi ni Phenobarbitone , Phenytoin na Carbamazepine. Hata hivyo   kuna kipindi huwa kunatokea changamoto za kukosekana kwa dawa hizi kwa baadhi ya maeneo, ambapo inapobainika hushughulikiwa.
Zipo changamoto katika kutoa elimu kwa pande zote mbili kwa upande wa wahudumu wa afya na jamii kwa ujumla ili maisha ya watu yasikatishwe kwa sababu ya ugonjwa huu hapa nchini.
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na Chama cha wataalamu wa ugonjwa  wa kifafa Tanzania tunaendelea kufanya kazi pamoja katika kuimarisha afya za wale wanaoishi na ugonjwa huu kwa kuwapatia elimu maalumu ya afya dhidi ya ugonjwa wa kifafa.
Jamii inapaswa kutambua na kuelewa kuwa Hospitali ndio sehemu sahihi pa kwenda  pale wanapokuwa na dalili za ugonjwa huu. Kifafa ni ugonjwa au tatizo la mfumo wa fahamu linalosababishwa na magonjwa mengi na unatibika.  Hivyo tushirikiane pamoja kuhamasisha watu wenye matatizo haya wanafika kwenye vituo vya kutolea huduma za afya ili kupatiwa matibabu husika.
KIFAFA KINATIBIKA, WAHI UPATE MATIBABU SAHIHI.
Imetolewa na ;
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
14/2/2017

No comments:

Post a Comment