Katika kuhakikisha Mkoa wa Rukwa
Upo salama kutokana na maambukizi ya ugonjwa wa Ebola yatakayoweza
kujitokeza, Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote
Stephen amefanya ziara ya siku tatu katika mwambao wa ziwa Tanyangika
kwenye Kata ya Kirando, Kabwe na Kasanga vijiji ambavyo vipo jirani na
nchi ya DRC ili kujionea namna Halmashauri ya Nkasi na Kalambo
zilivyojipanga kuhakikisha kuwa ugonjwa huo hautii mguu katika Mkoa na
nchi kwa ujumla.
Ziara hiyo aliianza siku ya
Ijumaa tarehe 26 hadi 28. 05. 2017 mara baada ya kumaliza kumalizika kwa
mafunzo ya siku tatu yaliyohusu utumaji wa taarifa za magonjwa kwa
kieletroniki (e-idsr) yenye kusisitiza tahadhari ya ugonjwa wa ebola
uliopo katika nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC)
yaliyotolewa kwa wahudumu wa afya wa Serikali na Sekta binafsi kwa
Halmashauri mbili za Manispaa ya Sumbawanga na Sumbawanga vijijini.
Mafunzo ya awamu ya pili
yanatarajiwa kumalizika tarehe 31. 05. 2017 kwa Halmashauri za Kalambo
na Nkasi ikiwa ni muendelezo wa awamu ya kwanza kwa Halmashauri ya
Sumbawanga Vijijini na Manispaa ya Sumbawanga yaliyoisha tarehe 26.
Mwezi wa tano.
Ili kujiridhisha na maandalizi ya
Halmashauri zinazopakana na nchi za jirani yaani Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo (DRC) pamoja na Zambia Mkuu wa Mkoa alipita katika
bandari maarufu za pwani ya ziwa Tanganyika na kuongea na vyombo vya
usalama ikiwemo uhamiaji, Sumatra, TRA, jeshi la polisi, jeshi la
wananchi, maafisa forodha pamoja na maafisa afya kutoka Wilayani.
Pia Mh. Zelote aliongea na
viongozi wa serikali za vijiji na kata wakiwemo madiwani, watendaji wa
kata na vijiji, wenyeviti wa vijiji na vitongoji, maafisa ugani wa kata
na vijiji, maafisa afya wa kata na vijiji na kufanya mikutano ya hadhara
ili kuwapa wananchi ujumbe aliokwenda nao katika kuhakikisha ugonjwa
huo haunusi katika mkoa wa Rukwa na nchi ya Tanzania.
Pamoja nae Mheshimiwa Mkuu wa
Mkoa aliambatana na Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt. Boniface Kasululu, Mratibu
wa Chanjo Mkoa Gwakisa Pamoja na Afisa kutoka Wizara ya Afya wa
usimamizi na ufuatiliaji Solomon Mushi, Mkuu wa Wilaya, makatibu tawala
wa wilaya pamoja na kamati za ulinzi na usalama za Wilaya.
No comments:
Post a Comment