Mkuu wa wilaya ya Mbogwe bi Martha
Mkupasi amewataka wananchi wa Mbogwe watoe ushirikiano wa kutosha kwa
Mradi Pendekezwa wa ujenzi wa Bomba la Kusafirishia Mafuta Ghafi
(EACOP) linalotarajiwa kujengwa kutoka Ziwa Albert kupitia Kabaale
(Uganda) hadi Rasi ya Chongoleani iliyo karibu na Bandari ya Tanga
nchini Tanzania.
Mkuu wa wilaya ameyasema hayo
alipofungua kikao cha maoni ya wadau (scoping) kwa Wakuu wa Idara na
watendaji wa kata wa Halmashauri ya wilaya ya Mbogwe kuhusu Tathmini ya
Athari kwa Mazingira na Jamii (TAM) ya mradi wa EACOP. Akiongea
wakati wa ufunguzi bi Martha amesema mradi huo utaleta maendeleo kwa
wanambogwe wote hivyo ni jukumu lao kuulinda .
Mradi wa Ujenzi wa Bomba la
Kusafirishia Mafuta Ghafi kutoka Uganda (Ziwa Albert) hadi Tanzania
(Tanga) lenye urefu wa kilometa 1445 linatarajiwa kupita katika wilaya
ya Mbogwe. Akiongea wakati wa kikao hicho ,mwezeshaji kutoka kampuni ya
JSB Envi-Dev Ltd Dr. Godfrey Kamukara ameelezea faida
zitakazopatikana kutokana na mradi huo zikiwemo upatikanaji wa ajira kwa
wakazi wa Mbogwe . Hata hivyo alitahadharisha kuwa mradi huo
unatarajiwa kusababisha mwingiliano wa makabila mbali mbali hivyo
kuwataka watendaji hao wawaelimishe wananchi kujikinga na maradhi
ikiwemo ugonjwa wa ukimwi.
Dr.Kamukara amewataka watendaji
kuwaelimisha wananchi kuhusu mafuta ghafi ili wananchi wasitoboe bomba
wakidhani ni mafuta yanayofaa kwa matumizi . Alieleza kuwa mafuta ghafi
ni mafuta ambayo bado hayajasafishwa kwa matumizi ya kawaida.
Kampuni ya RSK ya Uingereza na
washirika wake kutoka Uganda ( ECO partners ) na Tanzania ( JSB Envi-Dev
Ltd) wameanza kazi ya Tathimini ya Athari kwa Mazingira na Jamii kwa
kushirikisha jamii yote inayopitiwa na mradi kwa kutoa maoni ya mambo
muhimu ya kuzingatiwa wakati wa utekelezaji wa mradi huo
No comments:
Post a Comment