Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa
na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe (kulia) akimpa mkono wa
kumkaribisha nyumbani mchezaji wa Serengeti Boys Bw. Abdul Sulemani
(kushoto) katika hafla ya kuwapokea wachezaji hao waliorejea nchini
kutoka katika michuano ya AFCON nchini Gabon jana Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa
na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe (katikati waliokaa) akiwa katika
picha ya pamoja na wachezaji wa Serengeti Boys pamoja na viongozi wa
timu hiyo katika hafla ya kuwakaribisha baada ya kurejea kutoka katika
michuano ya AFCON nchini Gabon jana Jijini Dar es Salaam.
Wachezaji wa timu ya vijana chini
ya miaka 17 “Serengeti Boys” wakimsikiliza Waziri wa Habari Utamaduni
Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe (hayupo katika picha)
katika hafla ya kuwakaribisha baada ya kurejea kutoka katika michuano
ya AFCON nchini Gabon jana Jijini Dar es Salaam.
(Picha na: Lorietha Laurence – WHUSM
………………………
Na Shamimu Nyaki-WHUSM
Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa
na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe ameipongeza timu ya vijana chini
ya miaka 17 “Serengeti Boys” kwa hatua nzuri waliyofikia katika
kiwango cha Soka la Afrika kwa kushika nafasi ya pili katika kundi B
walilokuwa wanacheza wakati wa michuano ya AFCON iliyomaliziki hivi
karibuni Mjini Gabon.
Pongezi hizo zimetolewa jana
Jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya kuipokea timu hiyo katika
viwanja vya ndege vya Kimataifa vya Mwalimu Nyerere ambapo Waziri
Mwakyembe aliwataka walimu na wachezaji hao kuendelea kujiandaa kwa
ajili ya mashindano mengine yaliyo mbele yao.
“Nimefurahi kwa hatua mliyoifikia
na watanzani wote wanawapongeza kwa kuwa mmeshindana kwa uwezo wenu na
kuirudisha Tanzania katika ramani ya soka baada ya kukaa nje ya michezo
ya AFCON kwa takribani miaka 30 alisema” Mhe Mwakyembe.
Aidha aliongeza kuwa hapo
walipofika wao ni mashujaa na Serikali inaahidi kushirikiana nao
katika kuhakikisha kuwa vipaji hivyo vinaendelezwa kwa ajili ya ngazi
nyingine za kisoka.
Naye Kocha wa Serengeti Boys Kim
Paulsen ameiomba Serikali na wadau wa michezo nchini kuendelea kuisadia
timu hiyo katika maandalizi mbalimbali ili kuipa motisha zaidi katika
kufanikisha ndoto ya Tanzania katika mchezo wa soka.
Kwa upande wake kapteni wa timu ya
Serengeti Boys Bw. Dickson Job amewashukuru watanzania kwa mchango
mkubwa walioutoa kwao katika maandalizi mpaka hapo walipofikia ingawa
hawakufanikiwa kurudi na ushindi.
“Mchezo una matokeo matatu
kushinda, kushindwa au kutoka sare ingawa hatukutarajia kushindwa kwa
kuwa tulitamani sana kurudi na ushindi kama ambavyo tuliwaahidi
watanzania ila mwaka huu bahati haikuwa yetu ila tunaahidi kuendeleza
mapambano katika hatua zijazo” alisema Bw. Job
Timu ya Serengeti Boys imerejea
nyumbani baada ya kumalizika kwa michuano ya AFCON ambapo watapumzika na
kuingia kambini kwa ajili ya kujiandaa na michuano inayofuata ya chini
ya miaka 20 inayounda timu ya Ngorongoro Heroes.
No comments:
Post a Comment