(Jovina Bujulu- MAELEZO)
Wizara ya Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto kupitia Mpango wa Taifa wa Chanjo imevuka
lengo la kutoa chanjo na kuimarisha huduma nyingine za afya nchini.
Huduma hizo ni pamoja na udhibiti magonjwa ya kuambukiza na yasiyo ya
kuambukiza, magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele,huduma ya afya ya
uzazi na mtoto, lishe, pamoja na utoaji wa elimu ya afya kwa umma.
Waziri mwenye dhamana na wizara
hiyo Mhe. Ummy Mwalimu amebainisha hayo hivi karibuni alipokuwa
akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa kipindi
cha Mwaka wa Fedha 2017/18 mjini Dodoma.
Aliendelea kusema kuwa wizara
yake imehakikisha kuwepo kwa chanjo za kutosha ambapo jumla ya
shilingi bilioni 18 zimetumika kununua na kusambaza chanjo kwa watoto na
makundi mengine katika mikoa na Halmashauri zote nchini.
“Utoaji wa huduma za uhakika wa
chanjo umewezesha nchi yetu kuwa miongoni mwa nchi zilizofanya vizuri
kwa kipindi cha mwaka 2016, ambapo tumeweza kuvuka lengo kwa kufikia
kiwango cha chanjo cha asilimia 97” alisema Ummy.
Aidha, Wizara imenunua magari
tisa (09) kwa ajili ya kusambaza chanjo na majokofu 317 ya kutunzia
chanjo hizo kwenye vituo vya huduma za afya nchini.
Katika kuhakikisha kuwa huduma
kwa wananchi inaboresha, Wizara ya Afya kupitia Mpango wa Taifa wa
Kudhibiti Magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele imeendelea kugawa
dawa za kingatiba. Dawa hizo ni pamoja na za matende, mabusha, usubi,
trakoma, kichocho na minyoo katika Halmashauri 71 zenye maambukizi ya
magonjwa hayo.
Huduma hiyo iliwezesha wananchi
milioni 14.3 kufikiwa na wagonjwa 805 katika Halmashauri za Temeke na
Ilala, jijini Dar es salaam na watu 100 kutoka mkoa wa Mwanza
walifanyiwa upasuaji wa mabusha na matende bila malipo.
Wizara pia imeendelea na
mapambano dhidi ya ugonjwa wa malaria kwa kusambaza dawa za kutibu na
vipimo vya kupima (MRDT) katika mikoa 26 ya Tanzania Bara, dozi za dawa
mseto na vitepe vya MRDT vya shiilingi milioni18 zimenunuliwa na
kusambazwa katika vituo vya afya.
Katika kuhakikisha ugonjwa wa
malaria unatokomezwa, wizara imeendelea kuhamasisha matumizi ya kipimo
cha MRDT na kunyunyiza dawa ya ukoka katika mikoa ya Kanda ya Ziwa ya
Kgera, Mwanza, Mara na Geita ambayo ina maambukizi makubwa ya malaria na
kugawa vyandarua milioni 2.6 vyenye viuatilifu katika Halmashauri ya
Kilombero mkoani Morogoro na Halmashauri zote za jijini Dar es salaam.
Akizungumzia hali ya ugonjwa wa
kifua kikuu, Waziri Ummy alisema kuwa kwa sasa huduma za matibabu ya
ugonjwa huo zimeimarishwa na kusogezwa karibu na wananchi kutoka
hospitali moja ya Kibong’oto hadi kufikia vituo 18. Huduma za maabara
pia zimeboreshwa kwa kuimarisha maabara za Kandaya-Mbeya,
Bugando-Mwanza, hospitali ya rufaa mkoa wa Dodoma na Kibong’oto mkoani
Kilimanjaro.
Kuhusu hali ya ugonjwa wa UKIMWI
nchini , Wazii Ummy alisema kuwa wizara yake imeendelea kutoa ushauri
nasaha na kuwahimiza wananchi kupima mara kwa mara ili kujua hali ya
afya zao ambapo kwa kipindi cha mwaka 2016 jumla ya watu milioni 7.4
walipata ushauri nasaha na kupima VVU.
Katika kupambana na magonjwa
yasiyoambukiza, waziri alisema kuwa wizara yake imeandaa Mkakati wa
Kitaifa wa kupambana na magonjwa hayo wa mwaka 2016-2020 ambao
ulizinduliwa Dodoma mwaka 2016.
Mkakati huu unafuatia ongezeko
kubwa la magonjwa hayo ambayo ni kisukari, shinikizo la damu na magonjwa
ya moyo. Ili wananchi waweze kukabiliana na magonjwa hayo, wizara
imeanzisha kampeni ya kitaifa ya kuhamasisha wananchi kufanya mazoezi,
kupima afya mara kwa mara na kuzingatia ulaji wa chakula unaofaa.
Katika kipindi cha mwaka jana ,
huduma ya afya ya uzazi na mtoto imeimarishwa kwa kuandaa Mpango Mkakati
wa miaka mitano wa 2016-2020 unaolenga kuboresha afya ya uzazi, watoto
na vijana na kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi hadi kufikia 292 kwa
kila vizazi hai 100,000 ifikapo 2020. Kwa sasa vifo hivyo ni 556 kwa
kila vifo hai 100,000.
“Katika kutekeleza mkakati huo,
wizara imezingatia maeneo makuu matatu ambayo ni hududma ya uzazi wa
mpango, huduma wakati wa ujauzito na huduma wakati wa kujifungua”.
Alisema waziri Ummy.`
Akizungumzia upatikanaji wa
huduma ya uzazi wa mpango Waziri Ummy alisema wizara yake imefanya
jitihada za kuhakikisha huduma hiyo inapatikana kwa watu wote
wanaostahili ambapo kwa kipindi cha July mwaka 2016 na Machi 2017, jumla
ya watu 357,244 wamefanikiwa kupita huduma kupitia hospitali za mikoa
na watu 2,509,280 walifanikiwa kupata huduma hiyo kupitia vituo vya
afya.
Aidha, Waziri alitoa wito kwa
wakina mama wajawazito kuhudhuria kliniki angalau mara nne katika
kipindi cha ujauzito na kuzuia vifo vitakanavyo na uzazi vinavyoepukika,
lengo la Serikali ni kufikisha asilimia 70 ya wanawake wajawazito
kuhudhuria kliniki na kupata huduma ifikapo 2020 ili kunusuru maisha ya
mama na mtoto.
No comments:
Post a Comment