Mabingwa watetezi Yanga wamerudi
kileleni mwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kutokana na ushindi wa
mabao 2-1 dhidi ya Mbeya City ya Mbeya jioni ya jana Uwanja wa Taifa, Dar
es Salaam.
Ushindi huo unawafanya mabingwa hao watetezi watimize pointi 65
baada ya kucheza mechi 28 na kuendelea kuongoza Ligi Kuu. Simba
inaangukia nafasi ya pili kwa pointi zake 65 za mechi 29, ikizidiwa
wastani wa mabao.
Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Andrew Shamba wa Pwani,
aliyesaidiwa na Joseph Pombe wa Shinyanga na Haji Mwalukuta wa Tanga,
dakika 45 za kipindi cha kwanza zilimalizika Yanga ikiwa inaongoza 1-0.
Bao hilo lilifungwa na winga Simon Happygod Msuva kwa kichwa dakika ya saba tu akimalizia krosi ya Hassan Kessy.
Hata hivyo, Msuva hakuweza kushangilia bao hilo, kwani wakati
anaenda hewani kuunganisha krosi ya Niyonzima aligongana na beki wa
Mbeya City, Tumba Lui na kuchanika juu ya jicho la kulia.
Msuva hakuweza kuendelea na mchezo na kupelekwa kwenye zahanati
ndogo ya Uwanja wa Taifa kwa matibabu zaidi nafasi yake ikichukuliwa na
beki Juma Abdul.
Kwa mabadiliko hayo, Kessy alikwenda kucheza kama winga wa
kulia na Abdul akacheza beki ya kulia, ingawa walikuwa wakipokezana
kuzuia na kushambulia.
Kipindi cha pili Mbeya City walikianza vizuri na kufanikiwa
kupata bao la kusawazisha lililofungwa na beki wake wa kulia, Haruna
Shamte dakika ya 57 akitumia mwanya wa mabeki wa Yanga kupoteana.
Hata hivyo, Yanga wakafanikiwa kupata bao la pili lililofungwa
na mshambuliaji Mzambia, Obrey Chirwa dakika ya 64 akimalizia mpira wa
adhabu wa Juma Abdul.
Mbeya City ilijitahidi kujaribu kusawazisha bao hilo, lakini
tayari wapinzani wao, Yanga walikuwa wamekwishaanza kucheza kwa kujihami
zaidi na kushambulia kwa kushitukiza.
Mrisho Ngassa aliingia kipindi cha pili upande wa Mbeya City,
lakini hakuwa na madhara kwa timu ya timu yake ya zamani zaidi tu ya
kusisimua mashabiki kwa uchezaji wake mzuri.
Matokeo mengine ya mechi zilizochezwa leo
Kagera Sugar 2-1 Mbao FC
JKT Ruvu 0-1 Majimaji
Tanzania Prisons 2-1 Ndanda FC
Mtibwa Sugar 4 -2 Mwadui FC
No comments:
Post a Comment