Mahakama
ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam imeuagiza upande wa
Jamhuri kukamilisha kwa haraka upelelezi wa kesi ya vigogo watatu wa
Shirikisho la Soka (TFF), akiwamo aliyekuwa rais Jamal Malinzi, ili haki
iweze kutendeka kwa pande zote mbili. Uamuzi huo ulitolewa jana na
Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri.
Hakimu
Mashauri alisema ni aibu kila tarehe ya kesi inapopangwa upande wa
Jamhuri kudai upelelezi bado haujakamilika huku washtakiwa wakiwa
mahabusu zaidi ya miezi tisa sasa.
"Washtakiwa
wako mahabusu miezi tisa sasa imepita bila ya upelelezi kukamilika,
upande wa Jamhuri kamilisheni upelelezi haraka ili pande zote mbili
ziweze kupata haki," aliagiza Hakimu Mashauri.
"Mahakama
yangu inatupilia mbali (hata hivyo) maombi ya utetezi ya kwamba ina
mamlaka ya kuwaachia (huru) washtakiwa chini ya kifungu cha 225 kidogo
cha (5) cha sheria ya Mwendo wa Makosa ya Jinai (CPA)."
Akifafanua
uamuzi wake huo, hakimu huyo alisema mahakama hiyo kisheria haina
mamlaka ya kuwaachia washtakiwa hao kwa sababu miongoni mwa mashtaka
yanayowakabili ni ya kughushi ambayo hayaingii katika kanuni ya
kukamilisha upelelezi ndani ya siku 60.
Mbali
na Malinzi (58), washtakiwa wengine ni aliyekua Katibu Mkuu, Mwesigwa
Selestine(47) na Mhasibu, Nsiande Mwanga (28) wote wa TFF.
Wakati
huo huo, wakili wa utetezi Kashindye Thabiti alidai mahakamani hapo
kuwa hukosa ruhusa ya kuzungumza na washtakiwa wanapokwenda mahabusu ya
Magereza.
"Mheshimiwa
tunaomba mahakama yako itusaidie kupata kibali cha kuwaona washtakiwa
kwa sababu wateja wetu wana haki ya kuongea na mawakili ili kuwapa
mwongozo dhidi ya kesi yao," alidai Thabiti.
Wakili
wa serikali, Upendo Temu alijibu hoja ya utetezi kwa maelezo ufuate
utaratibu uliowekwa na Jeshi la Magereza wa kuwaona washtakiwa walioko
mahabusu.
Hakimu
Mashauri alisema katika kutembelea mahabusu waliopo magereza ni lazima
utaratibu uliowekwa na jeshi hilo ufuatwe. Alisema kesi hiyo itatajwa
Machi 28.
Machi
8, mwaka huu upande wa utetezi ulilalamika mahakamani hapo kuwa kesi
hiyo imechukua muda mrefu tangu washitakiwa walipofikishwa kwa mara ya
kwanza Juni, mwaka jana.
Malinzi
na wenzake walipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza Juni 29
wakikabiliwa na mashtaka 28 ikiwamo ya kughushi na kutakatisha fedha
dola za Marekani 375,418.
No comments:
Post a Comment