Naibu
Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye, ametoa
miezi miwili kwa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), kuhakikisha
linakamilisha uboreshaji wa jengo la abiria lililopo katika kiwanja cha
ndege cha Dodoma ili kuwezesha jengo hilo kuhudumia abiria wengi zaidi
kwa wakati mmoja.
Ametoa
agizo hilo, mkoani Dodoma katika hafla ya utiaji saini mkataba wa
uboreshaji wa jengo baina na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Nchini (TAA)
na NHC na kusema kuwa kukamilika kwake kutawezesha abiria zaidi ya 100
kuhudumiwa kwa wakati mmoja ambapo kwa sasa jengo linahudumia abiria 35.
“Mkataba
tunaoshuhudia ukisainiwa leo unaitaka NHC kukamilisha mradi huu ndani
ya miezi mitatu lakini niagize mradi huu ukamilike ndani ya miezi miwili
kwa sababu fedha zipo na cheti mlichonacho cha daraja la kwanza
kinaonyesha namna mnavyoweza kufanya kazi hii kwa haraka’ alisema
Mhandisi Nditiye.
Aidha
Naibu Waziri Mhandisi Nditiye ameitaka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege
Nchini (TAA), pamoja na maboresho hayo kuhakikisha inafanya maboresho
kwa kujenga maduka ya kubadilishia fedha na bidhaa ili abiria
watakaotumia kiwanja hicho hiyo waweze kupata huduma mbalimbali wakati
wanaposubiria kupanda ndege.
Ameongeza
kuwa Mkoa wa Dodoma kwa sasa ndio Makao Makuu ya Serikali hivyo miradi
yote inayotekelezwa chini ya Wizara lazima izingatie viwango na thamani
ya fedha ili kuendana na hadhi ya mji.
Kwa
upande wake Naibu Waziri wa Kazi, Vijana na Ajira ambaye pia ni Mbunge
wa Dodoma Mjini, Mheshimiwa Antony Mavunde ameipongeza Serikali kwa
kutekeleza mradi huo na kumuomba Naibu Waziri wa Uchukuzi na
Mawasiliano, kuwafikiria wananchi waliopisha upanuzi wa kiwanja hicho
kwa kuwalipa fidia mapema.
Naye
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya
Ujenzi), Mhandisi Joseph Nyamuhanga amesema Serikali inaendelea na
mipango ya kuboresha viwanja vya ndege mbalimbali hapa nchini ili
kurahisisha huduma za usafiri wa anga.
Ameongeza
kuwa Serikali imepanga kujenga Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa katika
eneo Msalato ambapo kwa sasa wataaalam wanapitia usanifu wa kiwanja
hicho na wakati wowote zabuni itatangazwa ambapo kiwanja hicho kitaweza
kuhudumia ndege kubwa za kisasa kwani kinatarajiwa kuwa barabara ya
kuruka na kutua ndege yenye urefu wa Kilomita 4.5 mpaka 5.
Awali
akitoa taarifa yake kabla ya utiaji saini Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya
Viwanja vya Ndege Nchini (TAA), Richard Mayongela, amesema kuwa Fedha
zinazotumika kukarabati jengo hilo ni fedha za ndani za mamlaka hivyo
jengo hilo litakamilika kwa wakati na viwango.
Uboreshaji
wa jengo la abiria lililopo katika Kiwanja cha Ndege cha Dodoma
utagharimu takribani kiasi cha shilingi milioni 600 na utahusisha mifumo
ya kisasa ya Tehama, mifumo na maji taka , mifumo ya matangazi ya
ratiba za ndege pamoja na mgahawa.
Imetolewa na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
No comments:
Post a Comment