Na Veronica Simba – Mara
Kamati
ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imetembelea na kukagua Mgodi wa
Buhemba na ule wa CATA Mining Ltd iliyopo mkoani Mara ikiwa katika
ziara ya kazi Machi 15 mwaka huu.
Katika
Mgodi wa Buhemba, Kamati ilielezwa kuwa, Serikali iliukabidhi Mgodi huo
wa dhahabu kwa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) mwaka 2011 ili
iuendeleze, kutoka kwa mmiliki wake wa awali ambaye ni Kampuni ya
Meremeta Limited.
Mkurugenzi
Mtendaji wa STAMICO Kanali Mhandisi Sylivester Ghuliku, aliieleza
Kamati kuwa Shirika limekamilisha upembuzi yakinifu katika mabaki ya
dhahabu yaliyoachwa kipindi cha nyuma ambapo umebaini kuwapo takribani
tani 796,400 za mabaki ya mchanga wa dhahabu yenye wastani wa kilo 852
za dhahabu.
“Aidha,
upembuzi huo ulibaini kuwa mabaki hayo ya mchanga yatachenjuliwa kwa
kutumia teknolojia ya Carbon in Leach (CIL). Mtambo unatarajiwa
kuchakata mabaki ya mchanga wa dhahabu kiasi cha tani 246,240 kwa
mwaka,” alisema.
Aliongeza
kuwa, tathmini ya kiuchumi ya mradi imeonesha gharama za uwekezaji
zinakadiriwa kufikia Dola milioni 3.96 na kwamba gharama za uendeshaji
kwa mwaka zinakadiriwa kufikia Dola milioni 4.46 na kutarajiwa kuingiza
faida inayofikia Dola milioni 3.45 kwa mwaka.
Kuhusu
tathmini ya mashapo katika miamba migumu, Kamati ilielezwa kuwa taarifa
za kitaalam zinaonesha kwamba wakati Kampuni ya Meremeta inafunga
uzalishaji katika mgodi, kiasi cha wakia 600,000 zilisalia kwenye miamba
migumu.
Akifafanua
zaidi, alisema kuwa STAMICO imeamua kufanya upya tathmini ya mashapo
hayo ili kujiridhisha. “Hadi sasa kiasi cha mashapo yenye wakia 441,772
kimethibitika kuwemo kwenye miamba migumu kutoka katika migodi ya wazi.
Ukadiriaji wa mashapo unaendelea,” alisema.
Vilevile,
ilielezwa kuwa Shirika lilifanikiwa kuchoronga shimo moja katika eneo
la Nyasanero ili kutathmini mkanda mpya wa dhahabu. Tathmini kamili ya
kiasi cha dhahabu kilichopo kwenye mwamba itakamilika mara baada ya
kupokea majibu ya maabara.
Akieleza
zaidi, alisema kuwa Januari mwaka huu, Shirika lilitangaza zabuni ya
kumpata mbia wa kushirikiana naye katika kuendesha mradi kwa njia ya
ushindani. Alisema, tayari Kampuni tatu zimenunua zabuni husika na
kwamba uchambuzi wa zabuni hizo unaendelea.
Katika
Mgodi wa CATA Mining Company Limited, Kamati ilielezwa kuwa Mgodi huo
unamilikiwa kwa ubia kati ya Mtanzania, Mahuza Mumangi na Raia wa Canada
Stefan Nagy kwa uwiano wa asilimia 50 kwa 50.
Akitoa
taarifa kwa Kamati ya Bunge kuhusu Mgodi huo, Kamishna Msaidizi wa
Madini, Ofisi ya Madini Musoma, Samwel Mayuki alisema kuwa Kampuni
inamiliki leseni sita za uchimbaji mdogo katika eneo la Kataryo ambapo
kuna miundombinu mbalimbali ikiwemo mitambo ya kusaga na kuchenjua
madini.
“Kuanzia
Julai 2016 hadi Juni 2017, Mgodi umezalisha kilo 241.3 za dhahabu zenye
thamani ya Dola 8,880,240.57 sawa na wastani wa shilingi bilioni 19.5
za Tanzania. Mrabaha uliolipwa ni Dola 355,209.66 sawa na shilingi
milioni 781 za Tanzania,” alisema Mayuki.
Aidha,
Kamishna Mayuki aliongeza kuwa, kwa kipindi cha kuanzia Julai hadi
Novemba 2017 Mgodi umezalisha kilo 62.4 za dhahabu zenye thamani ya Dola
2,239,659.86 sawa na shilingi bilioni 4.9 za Tanzania. Kiasi cha
mrabaha na ada ya ukaguzi wa madini kilicholipwa ni Dola 134,388.56 na
Dola 22,396.57 sawa na wastani wa shilingi milioni 295.7 za mrabaha na
milioni 49.3 za ada ya ukaguzi.
Vilevile, alisema Mgodi umeajiri jumla ya wafanyakazi 351 ambao kati yao 318 sawa na asilimia 91 ni watanzania.
Hata
hivyo, ilielezwa kuwa changamoto kubwa inayoukabili Mgodi kwa sasa ni
kusimamishwa kwa shughuli za Mgodi kuanzia Juni 2017 kutokana na mgogoro
baina ya wawekezaji husika na Jeshi la Wananchi wa Tanzania ambao ni
wamiliki wa eneo hilo la uchimbaji.
“Hali
hiyo imesababisha hasara mbalimbali ikiwemo kusimama kwa ajira za
watanzania 318, kushindwa kurejesha mikopo ya Benki na hasara ya
kupoteza mapato ya mamilioni ya shilingi kutokana na kusimama kwa
uzalishaji.”
Kamati
iliiagiza Wizara kuhakikisha inasaidia katika kushughulikia mgogoro huo
ili shughuli za uzalishaji katika Mgodi zirejee mapema.
Viongozi
mbalimbali wa Wizara walishiriki ziara hiyo wakiongozwa na Naibu Waziri
wa Madini Stanslaus Nyongo, ambaye aliahidi kwa niaba ya Wizara
kutekeleza maagizo yaliyotolewa na Kamati.
Naibu
Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo (kulia) akiwaeleza wajumbe wa Kamati
ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, mambo kadhaa kuhusu Mgodi wa
Dhahabu wa CATA Mining uliopo Mara, walipotembelea Mgodi huo wakiwa
katika ziara ya kazi Machi 15 mwaka huu.
Naibu
Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini
Profesa Simon Msanjila (kushoto) wakishiriki katika ziara ya Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, katika Mgodi wa CATA Mining mkoani
Mara, Machi 15 mwaka huu.
Wajumbe
mbalimbali wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini,
wakizungumza wakati wa ziara ya kamati hiyo katika Migodi ya Madini ya
Buhemba na CATA Mining iliyopo mkoani Mara, Machi 15 mwaka huu.
No comments:
Post a Comment