Katika
kudumisha haki za binadamu na utawala wa sheria nchini Tanzania, Kituo
cha Sheria na Haki za Binadamu kimeendelea kufanya uangalizi wa utendaji
kazi wa serikali ili kuhakikisha inatekeleza majukumu yake bila kukiuka
misingi ya haki za binadamu na utawala wa sheria.
Mnamo
Machi 7, 2018 Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kilipata taarifa za
kushtusha za kutokuonekana kwa Mwenyekiti wa Mtandao wa Wanafunzi
Tanzania (TSNP) Ndugu Abdul Nondo na kufarijika baada ya kupata taarifa
za kupatikana kwake mapema.
Hata
hivyo taarifa za shutuma zilizoelekezwa kwa Abdul Nondo kutoka kwa
jeshi la Polisi, Waziri wa Mambo ya Ndani pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Dar
es Salaam baada ya kujisalimisha kwa Jeshi la Polisi huko Iringa
zimekishitua Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu na kuona ni vyema
kufanya kumbushi ya kisheria kwa jeshi la polisi na viongozi hao kwa
kukiuka sheria kama inavyofafanuliwa;
Dhana ya Kutokuwa na Hatia (Presumption of Innocence)
Kwa
mujibu wa Ibara ya 13 (6) (b) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ya mwaka 1977, Sura No.2 kama ilivofanyiwa marejeo mwaka 2002:-
“Ni
marufuku kwa mtu yeyote aliyeshtakiwa kwa kosa la jinai kutendewa kama
mtu mwenye kosa hilo mpaka itakapothibitika kuwa anayo hatia ya kutenda
kosa hilo.”
Ni
kosa kumhukumu mtu yeyote bila ya chombo chenye mamlaka hayo
kuthibitisha kuwa mtu huyo amefanya kosa hilo. Viongozi wa kisiasa na
serikali kuzungumza baadhi ya masuala kama maamuzi ya mwisho na
kuingilia muhimili wa mahakama na kuwaita watu wahalifu na kusahau dhana
pana ya kutokuwa na hatia hadi imethibitishwa ni ukiukwaji wa Katiba.
Kuingiliwa kwa muhimili wa Mahakama
Mahakama
ndio chombo chenye mamlaka ya juu zaidi katika utoaji haki kama
ilivyofafanuliwa katika Ibara ya 107A (1) ya Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977:-
“Mamalaka yenye kauli ya mwisho ya utoaji haki katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Mahakama.”
Viongozi
wa serikali na jeshi la polisi watafanya kosa kumshutumu mtu yeyote
yule na kuingilia uhuru na kazi ya mhimili wa Mahakama kinyume cha
Katiba walioapa kuilinda.
Ukiukwaji wa Haki ya Kupata Dhamana
Katiba
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzanaia imetoa haki ya mtu kupata dhamana
pale ambapo suala lake lipo katika vyombo vya utaoji wa haki. Ibara ya
13 (6) (a) inaeleza:-
“Wakati
haki na wajibu wa mtu yeyote inapohitajika kufanyiwa maamuzi na
mahakama au chombo kingine chochote kinachohusika, basi mtu huyo atakuwa
na haki ya kupewa fursa ya kusikilizwa kiukamilifu, na pia haki ya
kukata rufani au kupata nafuu nyingine.”
Wakati
Jeshi la Polisi likiendelea na uchunguzi lilipaswa kutoa dhamana kwa
Abdul Nondo. Mahakama imeweza kutangaza vipengele vya sheria
vinanvyokinzana na Katiba katika kumnyima mtuhumiwa kupata dhamana pale
ambapo shauri lake linapokuwa linasikilizwa au anapokuwa chini ya
upelelezi wa Jeshi la Polisi.
Tumeshuhudia
hivi karibuni Mahakama ya Rufani ya Tanzania katika kesi ya Mwanasheria
Mkuu wa Serikali dhidi ya Mtobesya, ambapo Mahakama imetangaza kifungu
namba 148 (4) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai Sura No. 20 kuwa
batili kwani kinampa mamalaka Mkurugenzi wa Mashtaka mtuhumiwa haki ya
kupata dhamana. Si sahihi kumuweka mtu kizuizini bila dhamana au
kufikishwa mahakamani kwa zaidi ya siku saba wakati sheria imeweka masaa
24 .
Haki ya kupata Uwakilishi
Mtu
anapokuwa ameshikiliwa na Jeshi la Polisi kama mtuhumiwa anayo haki ya
kupata mwanasheria ili aweze kumwakilisha mahakamani wakati wa
kusikiliza kesi. Ibara ya 13 (6) (b) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ya mwaka 1977, imeeleza kwamba wakati haki na wajibu wa mtu
yeyote inapohitajika kufanyiwa maamuzi na mahakama au chombo kingine
chochote basi mtu huyo atakuwa na haki ya kupewa fursa ya kusikilizwa
kiukamilifu na kuweza kupata nafuu au nafuu nyingine ya kisheria.
Mahakama
zimetoa tafsiri juu ya Haki ya Uwakilishi kwa mtuhumiwa yeyote.
Mtuhumiwa anapaswa kuelekezwa kuwa ana haki ya kupata haki ya uwakilishi
toka kwa Wakili haya yalisemwa katika kesi ya Thomasi Mjengi &
Wenzake dhidi ya Jamhuri 1992 TLR 157, ambapo Jaji Mwalusanya enzi za
uhai wake alisema:-
“Haki
ya uwakilishi inahusisha pia haki ya mtuhumiwa kuambiwa kuwa ana haki
ya kupata uwakilishi na hayo yasipofuatwa basi maamuzi ya awali
yaliyotolewa huwa batili.”
Kituo
cha Sheria na Haki za Binadamu hakiafiki kitendo cha Polisi chini ya
kitengo cha Mkurugenzi wa upelelezi wa makosa ya jinai (DCI),
kuwakatalia Mawakili kuweza kumwona mtuhumiwa Abdul Nondo na kuweza
kupata haki ya uwakilishi mbele ya vyombo vya utoaji haki.
Msimamo wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu
Ili
kudumisha utawala wa sheria na haki za binadamu nchini, Kituo cha
Sheria na Haki za Binadamu kinawataka viongozi wa serikali na vyombo vya
dola kufuata sheria na kuheshimu haki za binadamu katika utekelezaji wa
majukumu yake.
Kituo
cha Sheria na Haki za Binadamu kinaitaka Tume ya Haki za Binadamu na
Utawala Bora (CHRAGG) kutumia mamlaka iliyopewa kwa mujibu wa sheria
kuwachukulia hatua viongozi wanaokiuka misingi ya haki za binadamu na
utawala bora.
Imetolewa Machi 15, 2018 na,
Dkt. Helen Kijo-Bisimba
Mkurugenzi Mtendaji
No comments:
Post a Comment