Utekelezaji
wa agizo la ujenzi wa viwanda 100 kwa kila mkoa uliotolewa na Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi),
Selemani Jafo, umefikia asilimia 49.4, viwanda 1,285 vikijengwa kati ya
2,600.
Akizungumza katika kikao kazi cha kupitia bajeti ya Tamisemi na mikoa mjini hapa jana, Jafo alisema viwanda hivyo vimejengwa ndani ya miezi mitatu tangu kutolewa kwa agizo hilo.
Alisema
agizo hilo bado linaendelea kutekelezwa na kila mkoa unatakiwa
kuhakikisha unajenga viwanda 100 kufikia Desemba 31, mwaka huu.
“Viwanda
hivi vilivyojengwa vina mchanganyiko mbalimbali vikiwamo viwanda
vikubwa, vya kati na vidogo, mna mikakati mikubwa ambayo itawezesha kuwa
na mchanganyiko wa viwanda vikubwa na vidogo,” alisema Jafo.
Alibainisha
kuwa kupitia wakuu wa mikoa, ajenda ya Rais John Magufuli ya Tanzania
ya Viwanda inatekelezwa na kuwataka waendelee kuitekeleza.
Awali
wakuu wa mikoa walitoa taarifa zao za ujenzi wa viwanda hivyo kufuatia
agizo alilolitoa huku Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda,
akibainisha kuwa katika mkoa wake tangu kutolewa kwa agizo hilo, viwanda
88 vimeshajengwa.
Hata
hivyo, Makonda alisema kumekuwa na changamoto ya umeme na maji na
kuiomba serikali kuliangalia suala hilo ili kuendelea kuvutia wawekezaji
zaidi.
Mkuu
wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo, alisema katika mkoa huo wamejenga
viwanda 22 ambavyo ni vikubwa na vya kati na vingine vipo katika hatua
mbalimbali za ujenzi.
“Changamoto iliyopo ni nishati ya umeme na kwa mkoa wetu tunahitaji tuwe na megawati 800,” alisema Ndikilo.
Mkuu
wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, alisema zimetengwa hekari 307,595 kwa
ajili ya uwekezaji wa viwanda na hadi sasa tangu kutolewa kwa agizo la
Jafo, vimejengwa viwanda 45 vipya ambavyo vimetoa ajira mbalimbali.
Mkuu
wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka, alisema mkoa wake unaendelea
kutekeleza mkakati wake wa bidhaa moja kwa wilaya moja na kwamba tangu
agizo hilo, viwanda 18 vipya vimejengwa.
Mkuu
wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza, alisema viwanda vipya vilivyojengwa
mkoani kwake ndani ya agizo hilo ni 124 huku Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga,
Zainab Tellack, akisema kwake amejenga viwanda 126.
No comments:
Post a Comment