Akizungumza na waandishi wa habari jana katika eneo la tukio Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Tabora Mhandisi Damian Ndabalinze alisema mvua zilizonyesha katika maeneo hayo zimesababisha kukatika kwa eneo hilo ambapo ndipo barabara ya lami inaishia.
Aliwataka madereva wa magari ya aina yoyote kudiriki kupita katika aina hilo kwa sababu wanaweza kuhatarisha maisha yao na abiria na mizigo.
Ndabalinze alisema dereva yoyote atakayekaidi na kuamua kupita katika eneo hilo kwa kulazimisha jambo lolote litakalompata itakuwa ni yeye kajisababishia na asilelekeze lawama kwa chombo chochote.
Alisema wakati taratibu nyingine zikiendelea za kutaka kurejesha mawasiliano kwa kutumia barabara hiyo ni vema magari yote ya kuja na kutoka Tabora yakapitia barabara ya Manyoni , Singida , Nzega hadi Tabora.
“Natoa wito kwa magari ya kwenda Kigoma na yale yanayoishia Tabora yapitie Nzega ili kuepusha usumbufu kwa abiria na kwa madereva …kwani njia hii haipitiki tena,” alisema Meneja huyo.
Naye Afisa Mfawidhi wa SUMTRA Mkoa wa Tabora Joseph Michael alisema kutokana na tatizo la kukatika kwa barabara hiyo anatoa ruhusa kwa magari yote yaliyokuwa yakipitia barabara ya Tabora kupitia Itigi hadi maeneo ya Dodoma na Dar es salaam kuzungukia Nzega bila kibali kwa siku ya leo.
Alisema baada ya hapo wamiliki wanatakiwa kutafuta vibali ikiwa kama hali ya barabara hiyo itachelewa ili kuepuka usumbufu.
Naye Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoani Tabora SP Emilian Kamuhanda alisema wamejipanga kutoka matangazo katika Stendi kuu ya mabasi Tabora na kushirikiana na Kikosi ya Usalama Barabara cha Mkoa wa Singida ili kuwaelekeza madereva wote wapiti njia ya Nzega ili kuepuka usumbufu.
Kwa upande wa Mtendaji wa Kata ya Kizenge Maganga Saulo alisema mvua iliyonyesha usiku wa kuamkia leo ilikuwa kubwa na kusababisha kukatika kwa eneo hilo , hatua iliyopelekea magari kushindwa kupita.
Alisema ili kuhakikisha hakuna maafa yatakayotokea wanatumia Jeshi la Akiba kuwazuia madereva wanaotaka kujaribu kuvuka.
Na Tiganya Vincent, Tabora
No comments:
Post a Comment