Siku
chache baada ya Naibu Waziri wa Habari Sanaa, Michezo na Utamaduni,
Juliana Shonza kusema wasanii waliofungiwa nyimbo zao wanatakiwa kufuata
taratibu kama wana malalamiko, msanii wa Bongo Fleva, Ibrahim Musa
maarufu Roma Mkatoliki amesema alifuata taratibu hizo lakini amegonga
mwamba.
Roma
ameyasema hayo jana Jumatano Machi 21, 2018 katika mahojiano na
kipindi cha XXL kinachorushwa na kituo cha Radio Clouds, akidai kuwa
adhabu ya kufungiwa miezi sita inamuumiza na kuomba apunguziwe au
kutozwa faini ili yaishe.
Machi
1, 2018 Shonza alimfungia Roma Mkatoliki kutojihusisha na tasnia ya
muziki kwa kipindi cha miezi sita na kwamba msanii huyo alipopewa muda
wa kurekebisha wimbo wake wa Kibamia, ameshindwa kutekeleza agizo hilo.
Katika
kipindi hicho, Roma amesema tangu siku alipofungiwa alijitahidi kufanya
taratibu za kumuona naibu waziri huyo kama ambavyo alitaka, ikiwemo
kufunga safari hadi ofisini kwake lakini hakufanikiwa.
Amebainisha
kuwa amefungiwa wakati tayari ana shoo za kufanya na alishachukua
fedha, ikiwemo shoo ya Kili Marathon ambayo baadaye alitakiwa kurejesha
fedha hizo.
“Shoo
ya Kili Marathon mimi na Stamina kupitia kundi letu la Rostam tulikuwa
tumelipwa vizuri, lakini juhudi za kufanikisha ziligonga mwamba hata kwa
kuomba barua kidogo ya utambulisho. Mambo kama haya yanatuharibia
kuaminika tena kwa kampuni ambazo zinatupa kazi,” amesema.
Kuhusu
kumuona naibu waziri amesema, “Siku moja nilitoka hospitali nikampitia
rafiki yangu Madee na Askofu nikawaambia twendeni tukamuone mheshimiwa
lakini mimi sikupewa ruhusa ya kumuona. Wengine wote walipewa ruhusa,
basi nikawatuma wao wafikishe ujumbe kwa sababu niliogopa kulazimisha
kwa kuwa ningeonekana nafanya fujo.”
Amesema
alitakiwa kupewa muda kabla ya hatua iliyochukuliwa kuliko kudhaniwa
kuwa anakaidi agizo la kutakiwa kuripoti ofisi za Baraza la Sanaa la
Taifa (Basata).
“Walitakiwa
kujua kuwa nilikuwa na udhuru na pia hiyo ilikuwa ni mara yangu ya
kwanza,” amesema na kubainisha kuwa hata kama alipigiwa simu, aliogopa
kupokea kwa sababu ya uoga alionao tangu alipotekwa na watu
wasiojulikana mwaka jana.
“Inaonekana
Roma hajafanya kitu chochote tangu litokee jambo hilo lakini ambacho
mimi sijafanya ni kuja kwenye media kusema leo nimeandika barua au vipi?
Sikupewa barua kwa wakati ule nilipewa ujumbe tena kwa namba ngeni.”
No comments:
Post a Comment