Mahakama
ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, imesema itaanza
kusikiliza ushahidi wa Jamhuri dhidi ya kesi inayomkabili Ofisa Msaidizi
wa Forodha wa Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA), Jennifer Mushi
anayekabiliwa na tuhuma za kumiliki magari 19 na kuishi maisha ya juu
kuliko kipato chake kama mtumishi yenye thamani ya zaidi ya Sh. milioni
530.8.
Kesi hiyo ilipangwa kusikilizwa jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shahidi.
Hata
hivyo, upande wa Jamhuri uliomba mahakama kupanga tarehe nyingine kwa
kuwa mashahidi hawajapatikana kutokana na kuwa na majukumu mengine.
Wakili
wa Serikali Vitalis Peter alidai kuwa kutokana na mashahidi kuwa na
majukumu mengine ya serikali wameshindwa kuwapata kwenda kutoa ushahidi
dhidi ya mshtakiwa huyo.
Hakimu alisema mahakama yake itaanza kusikiliza ushahidi wa Jamhuri Aprili 9.
Katika
kesi ya msingi, Peter alidai kati ya Machi 21, 2016 na Juni 30 mwaka
huo mahali tofauti jijini Dar es Salaam, akiwa mtumishi wa TRA,
mshtakiwa huyo alikutwa akimiliki mali zisizolingana na kipato chake,
kinyume na sheria ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(Takukuru).
Alitaja
mali hizo kuwa ni magari 19 ya Toyota Rav4, Toyota Dyna Truck, Toyota
Vitz, Suzuki Carry, Toyota Ipsum, Toyota Wish, Toyota Mark II, Toyota
Regius, Toyota Estima, Toyota Alex, Toyota Noah, Toyota Crown, Toyota
Hiace, Toyota Estima, Toyota Passo na Suzuki Carry, yote yakiwa na
thamani ya Sh. milioni 197.6.
Katika
shtaka la pili, ilidaiwa kati ya Machi 21, 2012 na Machi 30, 2016
jijini Dar es Salaam akiwa mwajiri wa TRA aliishi maisha ya hali ya juu
tofauti na kipato chake, yenye thamani ya Sh. 333,255,556.24.
Mshtakiwa alikana mashtaka hayo na yuko nje kwa dhamana.
No comments:
Post a Comment