Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amesema
kuwa anapokea mialiko mingi kutoka nje ya nchi lakini amesema hawezi
kusafiri kwenda huko kwasababu sio jimbo lake.
Akiwa ametimiza siku 859 madarakani, Rais John Magufuli ametembelea nchi chache huenda kuliko watangulizi wake wanne.
Magufuli
ametembelea Kenya, Uganda, Rwanda na Ethiopia katika kipindi chote cha
utawala wake huku akitimiza miaka miwili, miezi minne na siku saba tangu
aapishwe kuwa Rais wa Tanzania Novemba 5, 2015.
Huenda hilo lilimfanya jana atoe siri na sababu zinazomfanya asipende kusafiri mara kwa mara nje ya nchi.
Akiwa
mjini Singida jana alikozindua kiwanda cha mafuta ya kupikia cha Mount
Meru Millers Group, Rais Magufuli alisema amekataa zaidi ya mialiko 70
ya kwenda nje ya nchi kwa sababu hakuchaguliwa na Watanzania kwenda huko
bali kuwatumikia.
“Nataka
Tanzania yote niizungukie ndiyo maana sitaki kwenda nje, maana huko si
kwenye jimbo langu, jimbo langu mimi ni Tanzania. Nimekataa mialiko
zaidi ya 70. Niende nje kufanya nini wakati sijamaliza kutatua kero za
wananchi.”
“Nataka
nizitatue kero za wananchi walionipigia kura kwanza, walipanga foleni
wakati wa mvua na jua kunichagua mimi na waheshimiwa wabunge,” alisema Rais Magufuli.
“Bado sijaenda, Iringa, Mbeya, Rukwa na sehemu nyingine, lazima nizunguke nchi yote kutatua kero za wananchi..” alisema.
Julai
4, mwaka jana, alisema alipata mialiko zaidi ya 60 kwenda nje ya nchi
baada ya kuwa Rais, lakini aliikataa kwa sababu anataka kuishughulikia
Tanzania kwanza.
Alisema hayo akiwahutubia wakazi wa Sengerema katika uzinduzi wa mradi wa maji.
Alisisitiza
kuwa hana haja ya kwenda nje ya nchi kwa sababu bado ana mzigo mkubwa
wa kumaliza ufisadi. “Niende nje kufanya nini wakati nitaenda tu
nikishastaafu, nataka nimalize kwanza haya ya hapa ndani,” alisema pia
mwaka jana mjini Sengerema.
Alipozungumza
na watendaji mbalimbali wa Serikali Ikulu jijini Dar es Salaam Novemba
7, 2015, Magufuli alifuta safari za nje kwa watendaji wote wa Serikali
na kusisitiza kuwa kama kuna ulazima, mhusika atapaswa kupata kibali
kutoka kwa Katiba Mkuu Kiongozi.
Baadaye
akizindua bunge la 11, Novemba 20 mwaka 2015, Magufuli alisema kuanzia
mwaka 2013 hadi 2015, safari za nje zilikuwa zimeigharimu Serikali
Sh356.3 bilioni.
Jana,
Rais Magufuli katika uzinduzi huo wa kiwanda cha mafuta, aliagiza
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Wizara ya Viwanda, Biashara na
Uwekezaji kupandisha kodi kwa waingizaji wa mafuta ghafi ya chakula
kutoka nje ya nchi.
Alisema hatua hiyo itawezesha wawekezaji wa ndani wa viwanda vya mafuta ya chakula kupata soko.
Rais Magufuli alitoa agizo hilo wakati ambao Serikali inafanya maandalizi kwa ajili ya bajeti ya mwaka wa fedha wa 2018/19.
Alisema
anafahamu mchezo mchafu unaofanywa na waagizaji wa mafuta kutoka nje ya
nchi ikiwa ni pamoja na kuua soko la ndani la mafuta ya chakula.
“Ninafahamu
mchezo mchafu unaofanywa na waagizaji wa mafuta, wanapofanya hivyo
lengo lao si kutengeneza soko la ajira bali ni kuua soko la mafuta,”
alisema.
Rais
Magufuli alisema, “wanachofanya wanaagiza mafuta kwa kisingizio kuwa ni
crude oil (mafuta ghafi) yanayohesabika kama ni malighafi,” alisema.
Aliongeza
kuwa, kwa kisingizio hicho, TRA na watu wengine hawawatozi kodi na
wanapoyafikisha nchini waagizaji hao huyaweka kwenye madebe na kuyauza
hivyo kutengeneza faida kubwa.
“Nataka
mwaka huu... wabunge mko hapa na waziri uko hapa... na waziri wangu
najua mnanisikia nataka mafuta hayo yanayoagizwa kutoka nje yatandikwe
charge (gharama) kubwa sana,” aliagiza.
Alisema anafahamu waagizaji hao huwa wanajikusanya na kwenda bungeni kuzitembelea kamati za Bunge.
“Naomba wabunge na mawaziri msikubali lobbing (ushawishi) za namna hiyo, mnawaumiza wananchi,” alisema.
Rais
Magufuli alisema mahitaji halisi ya mafuta ya chakula kwa mwaka ni tani
450,000 na nchi inazalisha tani 135,000 sawa na asilimia 30, huku
asilimia 70 ya mafuta ikiagizwa kutoka nje.
Alisema wanapoagiza mafuta hayo wanatumia dola za Marekani, fedha ambazo zingeweza kutumika katika shughuli zingine.
Rais alisema mafuta ya chakula yanachukua nafasi ya pili ya bidhaa zinazoingizwa nchini kutoka nje.
“Lakini
mtu wa kawaida angeweza kutuuliza kweli Tanzania tuna wajibu wa kuagiza
mafuta, tutumie fedha yetu ya kigeni kununulia mafuta ya chakula?”
alihoji.
“Mtu
yeyote mwenye akili timamu atakushangaa, mimi ndugu zangu ni mtaalamu
wa kutengeneza mafuta nimewahi kukaa viwandani ninafahamu mchezo mchafu
wanaoucheza hawa waagizaji.”
Pia,
alimuagiza Waziri wa Viwanda, Charles Mwijage akamweleze mwenzake wa
Wizara ya Fedha, Dk Philip Mpango kuangalia namna wanavyoweza
kuwapunguzia gharama za kodi wawekezaji wa viwanda vya ndani.
“Haiingii
akilini kutoza Vat (Kodi ya Ongezeko la Thamani) na kutoza kodi zingine
kwa mtu ambaye ana kiwanda hapa; anatumia umeme wa hapa, anatumia maji
ya hapa, anatumia malighafi za hapa, ametengeneza mnyororo wa ajira
mkubwa wa watu wa hapa,” alisema.
Aliongeza
kuwa kiwanda kama hicho kitanunua umeme, hivyo Tanesco watachukua fedha
na Wizara ya Maji pia itapeleka maji kwenye kiwanda.
“Yale
maji yatalipiwa kodi na wakulima wataweza kuuza mazao yao na
wafanyabiashara nao watapunguza gharama za kusafirisha bidhaa zao sababu
kiwanda kipo karibu.”
No comments:
Post a Comment