Na Lucas Mboje, Jeshi la Magereza;
Jeshi
la Magereza limetiliana saini makubaliano na Asasi ya TECHNOSERVE
katika kuendesha mafunzo ya ujasiriamali kwa wafungwa vijana wenye umri
wa kati ya miaka 18 hadi 30 waliopo magerezani katika Mikoa ya nyanda
za juu Kusini ikiwemo Mbeya, Songwe, Iringa, Njombe, Ruvuma, Katavi na
Rukwa.
Hafla
ya kutiliana saini makubaliano hayo imefanyika katika Ofisi za Makako
Makuu ya Jeshi la Magereza jijini Dar es Salaam na Asasi ya TECHNOSERVE
iliwakilishwa na Afisa wake Bw. Monsiapile Kajimbwa.
Akizungumza
baada ya kutiliana saini makubaliano hayo, Kamishna Jenerali wa
Magereza, Dkt. Juma Malewa amesema kuwa mafunzo hayo ya ujasiriamali
yatawapa uwezo wafungwa wa kubaini na kutumia fursa mbalimbali za
kiuchumi ikiwemo uwezo wa kubuni na kuandaa mipango ya biashara.
“Mafunzo
haya yatawanufaisha sana wafungwa waliopo magerezani katika mikoa hiyo
kwani yatawajengea uwezo wa kujitambua pamoja na kujipatia vipato halali
badala ya kutenda uhalifu katika jamii.” Alisema Jenerali Malewa.
Ameongeza
kuwa mafunzo hayo yatafanyika katika Chuo cha Ufundi cha Magereza
Ruanda kilichopo Mkoa wa Mbeya ambapo wafungwa watajifunza nadharia na
vitendo katika dhana nzima ya ujasiriamali ikiwemo stadi za utengenezaji
sabuni, ushonaji, useremala, ufumaji sambamba na uandaaji wa mipango ya
kibiashara.
Meneja
Mkazi wa Asasi ya TECHNOSERVE, Bw. Monsiapile Kajimbwa amesema kuwa
hatua ya kutiliana saini makubalino hayo ni kuimarisha ushirikiano kati
ya Asasi yake na Jeshi la Magereza katika kutoa mafunzo kwa wafungwa ili
waweze kupata ujuzi kupitia program hiyo.
Dira
ya Jeshi la Magereza ni kuwa Jeshi la kurekebisha wahalifu lenye
utaalam wa hali ya juu linaloendeshwa katika kanuni na viwango
vilivyowekwa Kitaifa na Kimataifa.
No comments:
Post a Comment