Rais John Magufuli amesema matokeo ya uchunguzi uliofanywa na kamati yake teule yamebaini kuwapo viwanda hewa vilivyokuwa vinaagiza sukari ya viwandani.
Amesema
Machi 15, mwaka huu amepokea ripoti hiyo yenye idadi ya viwanda 30 huku
viwanda vinane tu ndiyo vikibainika kuwa na taarifa za kweli katika
uagizaji wa sukari.
Kampuni
hizo nane ni ASB, Nyanza Bottlers, Bonite Bottlers Ltd, Bakhresa Group
of Companies, Kazman Group, Lakailo Company, ANB Group na Kampuni ya
Super ASB.
Rais
Magufuli alibainisha hayo jana wakati wa Mkutano wa 11 wa Baraza la
Taifa la Biashara (TNBC) uliofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam, yeye
akiwa mwenyekiti wake.
"Niliunda
kamati maalum ya kufuatilia suala la uagizaji wa sukari kutoka nje,
nimepokea ripoti Machi 15, mwaka huu (Alhamisi)," alisema Rais Magufuli.
"Kilichobainika humo kinasikitisha sana, kampuni zaidi ya 22 zilikuwa
zinaagiza sukari kwa manufaa yao."
Rais
Magufuli alisema kamati hiyo imebaini kuwa kampuni hizo 22 zilikuwa
zinaagiza sukari kuliko mahitaji yao halisi waliyokuwa wanayahitaji.
Rais Magufuli alitolea mfano wa kampuni ya Iringa Food Products iliyokuwa imeagiza tani 300 wakati mahitaji yake ni tani 190.
Alisema
kuna kampuni ya Dabaga ilikuwa inaagiza tani 2,000 wakati mahitaji
halisi ni tani 1,600. Alisema kuna viwanda vimekuwa vikiagiza sukari ya
viwandani lakini huibadilisha kuwa ya matumizi ya binadamu badaye.
Sukari ya viwandani kutoka nje ya nchi ina unafuu mkubwa wa kodi ya forodha kulinganisha na ile ya kawaida.
Mwenyekiti
huyo wa TBNC alitoa takwimu hizo ikiwa ni malalamiko yake kwa sekta
binafsi ambayo awali ilikuwa imeorodhesha kero mbalimbali za upande wa
serikali zilizopo katika biashara na uwekezaji nchini.
Rais
Magufuli alisema kuna baadhi ya viwanda bado havijajengwa lakini
wamiliki wake wamekuwa wakiagiza hadi tani 500 na kueleza kuwa wahusika
wote waliobainika wataandikiwa barua.
"Kuna
kiwanda kinaitwa Maisha Bottlers kiliagiza tani za sukari 7,000
kikieleza kiko Mbeya," alisema mwenyekiti huyo, "lakini kamati (ya
uchunguzi) imeenda Mbeya, imekitafuta, haijakiona."Hii ripoti
nitamkabidhi Waziri Mkuu aipitie na achukue hatua."
Alisema
suala la sukari limekuwa likiwaweka watu wengi matatani wakiwamo
mawaziri wa tangu utawala wa Rais wa tatu, Benjamini Mkapa (1995-2005).
Alisema
mahitaji ya sukari nchini ni tani 590 kwa mwaka, ambapo tani 455 ni kwa
matumizi ya nyumbani na tani 135 kwa matumizi ya viwandani.
Aliongeza kuwa kwa sasa kuna upungufu wa tani 130 kwa sukari ya kula na tani 135 kwa matumizi ya viwandani.
No comments:
Post a Comment