NA WAMJW-DAR ES SALAAM.
WAZIRI
wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu
amewashauri wananchi kwenda vituo vya tiba haraka mara baada ya kugundua
kuwa wana dalili za ugonjwa wa dengue.
Hayo
ameyasema wakati alipotoa tamko juu ya kuingia kwa ugonjwa wa dengue
hapa nchini mara baada ya kufunga Mkutano wa 65 wa Jumuiya ya Mawaziri
wa Afya wa Nchi za Afrika Mashariki, Kati na Kusini ECSA jana jijini
Dar es salaam.
“Kuna
dalili za Ugonjwa Dengue zikiwemo homa ya ghafla, kuumwa kichwa hususan
sehemu za macho, maumivu ya viungo na uchovu. Dalili hizi huanza
kujitokeza kati ya siku 3 hadi 14 tangu mtu alipoambukizwa virusi vya
homa ya Dengue hivyo Wizara inashauri kuwa wananchi wasiwe na hofu, bali
mara tu wanapoona dalili za ugonjwa waende katika vituo vya tiba "
alisema Waziri Ummy.
Aidha
Waziri Ummy amesema kuwa Wakati mwingine dalili za ugonjwa huu zinaweza
kufanana sana na dalili za malaria hivyo basi wananchi wanaaswa kuwa,
wakipata homa wahakikishe kuwa wanapima ili kugundua kama wana vimelea
vya malaria au Dengue, au sababu nyingine, ili hatua stahiki
zichukuliwe.
Waziri
Ummy amesema kuwa ili kujikinga na ugonjwa huo ni lazima Kuangamiza
mazalio ya mbu kwa kufukia madimbwi ya maji yaliyotuama au nyunyuzia
dawa ya kuua viluwiluwi vya mbu kwenye madimbwi hayo pamoja na Kujikinga
na kuumwa na mbu kwa kuvaa nguo ndefu muda wote hasa nyakati za
mchana.
Aidha
Waziri Ummy amesema kuwa Wizara itaendelea Kuimarisha ufuatiliaji wa
magonjwa nchi nzima kwa kutumia mfumo uliopo wa ukusanyaji wa taarifa
(IDSR), ambapo tunaendelea kupata taarifa za kila siku juu ya mwenendo
wa ugonjwa huu na Kutoa elimu kwa jamii kupitia vyombo vya habari.
Mbali
na hayo Waziri Ummy amesisitiza kuwa hakuna vikwazo vyovyote
vilivyowekwa kwa ajili ya wasafiri wanaoingia na wanaotoka nchini na
Wizara itaendelea kushirikiana na wadau na sekta mbalimbali katika
kufuatilia na kudhibiti ugonjwa huo.
Homa
ya Dengue ni ugonjwa unaosababishwa na virusi vinavyoenezwa na mbu wa
aina ya Aedes ambao ni weusi wenye madoa madoa meupe yenye kung’aa.
No comments:
Post a Comment