Kiongozi
wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, amesema amejipanga kupeleka
bungeni mpango mbadala kuhusu sera za kibajeti akidai mpango wa bajeti
ya serikali umejikita kwenye maendeleo ya vitu badala ya maendeleo ya
watu.
Zitto
(41), ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Mjini aliyasema hayo jana jijini
Dar es Salaam alipozungumza na waandishi wa habari juu ya mrejesho wa
ziara yake aliyoifanya katika kata zinazoongozwa na chama chake, nchini
kote.
Alisema
mpango wake huo umelenga kuunda mpango mwingine mpya utakaosimamia
masuala ya uchumi shirikishi unaozalisha ajira pamoja na kuhakikisha
kilimo na viwanda vinavyoongeza mnyororo wa thamani ya mazao ya kilimo
vinapewa kipaumbele.
Vitu
vingine ambavyo alisema vinapaswa kupewa kipaumbele ni usalama wa
chakula na lishe pamoja na huduma bora za kijamii hususani maji, elimu
na afya.
"Juzi
serikali imeainisha vipaumbele vya kibajeti kwa mwaka 2018/19. Masuala
ya watu hususani kilimo, maji hayamo kwenye vipaumbele hivyo," Zitto
alisema na kufafanua zaidi:
"Ni
rai yetu kwa serikali ijitazame katika eneo hilo, ikae chini na kuja na
mpango mpya utakaojikita katika masuala ya watu na siyo kama mpango huu
wa sasa unaojikita kwenye vitu tu.
"ACT-Wazalendo
tutahakikisha tunaupinga bungeni mpango huu wa bajeti wa sasa ili
uandaliwe upya kwa sababu huu uliopo unawaacha kando kwa asilimia 70
Watanzania, tunataka tuwe na 'balance' (uwiano) ya vipaumbele vya
kujenga nchi na vya kujenga taifa ili tuhakikishe vitu vya muhimu kama
elimu, kilimo, afya na vitu vingine vinavyowahusu watu moja kwa moja
vinaguswa na kupewa kipaumbele."
Wiki
iliyopita serikali kupitia kwa Waziri wa Fedha na Mipango, Dk, Philip
Mpango iliwasilisha kwa wabunge mapendekezo yake kuhusu ukomo wa bajeti
na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa mwaka 2018/19.
Dk.
Mpango alisema bajeti ijayo ambayo itakuwa ya tatu kwa serikali ya
awamu ya tano inatarajia kuwa Sh. trilioni 32.476. Kati yake, Sh.
trilioni 20.468 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida, sawa na asilimia 63
ya bajeti na Sh. trilioni 12.007 zitatumika kwa shughuli za maendeleo,
sawa na asilimia 37 ya bajeti.
Waziri
huyo alisema miradi kielelezo itakayopewa msukumo ni pamoja na ujenzi
wa reli ya kati kwa kiwango cha standard gauge kiasi cha Sh. trilioni
1.4, kukamilisha malipo ya ununuzi wa ndege ya pili aina ya
Dreamliner-Boeing 787, ununuzi wa ndege moja mpya aina ya Bombadier Dash
8 Q400 na kuanza uendeshaji wa ndege mpya Boeing 787 na Bombardier CS
300, zikitengewa Sh. bilioni 495.6.
Pia
alisema Sh. bilioni 700 ambazo ni fedha za ndani zimetengwa kwa ajili
ya ujenzi wa kambi na ofisi za wafanyakazi, ujenzi wa bwawa na ujenzi wa
njia kuu za kupitishia maji katika mradi wa Stieglers' Gorge.
Katika
mkutano wake na waaandishi wa habari jana, Zitto ambaye aliwahi kuwa
mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), pia aliiomba serikali kuitisha
mkutano wa kitaifa wa maridhiano ya kisiasa kama jukwaa la kuzijadili
changamoto za uendeshaji wa siasa nchini.
Alisema
mkutano huo utasaidia kuondoa uadui unaoendelea kukua kwa sasa kati ya
serikali na wananchi, viongozi wa dini, mashirika yasiyo ya kiserikali,
taasisi za wanafunzi pamoja na vyama vya upinzani na anaamini mazungumzo
ya kitaifa ndiyo jambo sahihi la utatuzi wa suala hilo.
Kiongozi
wa ACT-Wazalendo huyo pia alipendekeza kuundwa kwa tume huru ya
kuchunguza matukio ya mauaji, utekwaji na kupotea kwa wafanyabiashara,
viongozi wa kisiasa, waandishi wa habari pamoja na wananchi wengine.
No comments:
Post a Comment