Kambi
ya siku tano inayoendeshwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul
Makonda kuwatafuta wanaume waliotelekeza watoto wao imempa umaarufu
mitandaoni msichana aliyejitambulisha kwa jina moja la Safina.
Picha
za msichana huyo ambaye ni mkazi wa Dar es Salaam, zilianza kusambaa
kwenye mitandao ya kijamii tangu alipoonekana nje ya ofisi za Mkuu wa
Mkoa juzi asubuhi akiwa na mtoto wake anayefanana na Mchina.
Mwanamke
huyo alipigwa picha akiwa amekaa kwenye ofisi hizo na mtoto wake huyo
akisubiri foleni ya kupata msaada kutoka kwa wanasheria, maofisa ustawi
wa jamii na polisi kutoka Dawati la Jinsia.
Baada
ya picha hiyo kusambaa iliibuka mijadala kwenye mitandao hiyo wengi
wakihoji kama kweli baba wa mtoto huyo atakuwa Mtanzania.
Baada
ya muda kupita, ujumbe wa video iliyomrekodi msichana huyo ulisambaa
akielezea alivyokutana na Mchina huyo na kuanzisha uhusiano ambao
hatimaye ulisababisha kupatikana kwa mtoto huyo.
Kwenye
ujumbe huo, msichana huyo alisema alikutana kwa mara ya kwanza na
mchina huyo mwaka 2013 alipokuwa akifanyakazi kwenye kampuni ya ujenzi
ya Hainan kutoka China.
Alisema
wakati huo kampuni hiyo ilikuwa ikijenga majengo maeneo ya Gongolamboto
jijini Dar es salaam na baadaye walihamia mkoani Dodoma na kuendelea na
maisha.
"Nilikaa
na baba yake huyu mtoto miaka mitatu mkoani Dodoma hadi alipopata
matatizo na kuamua kurudi kwao China.... aliniambia atarudi na
atanitafuta kwa njia ya simu lakini hadi leo sina mawasiliano naye,"
alisema.
Safina
alisema anamlea mtoto huyo katika mazingira magumu bila msaada kwa kuwa
mtoto huyo hana ndugu yeyote wa upande wa baba hapa nchini.
Safina
alikuwa akizungumza huku akionyesha picha mbalimbali zinazoonyesha
hatua za mahusiano yao, ikiwemo inayomwonyesha mzazi mwenzake akiwa
amembeba mtoto huyo alipokuwa mchanga huko mkoani Dodoma.
Pia
alikuwa akiwaonyesha waandishi wa habari vibali vya muda vya ukaazi
alivyokuwa akitumia raia huyo wa China alipokuwa akifanyakazi nchini
ambavyo vimeisha muda wake.
Msichana
mwingine ambaye ujumbe wake wa video umesambaa ni Mwajuma Mohamed
ambaye alisema kuwa ametelekezwa na mzazi mwenzake hivyo utaratibu
ulioanzishwa na Mkuu wa Mkoa ni ukombozi kwao.
Alisema
kwa sasa maisha ni magumu na kwamba ingawa yuko hai lakini anashindwa
kuyamudu na kuhoji kuwa itakuwaje kama ikitokea akafariki na kumwacha
mtoto wake bila baba.
Anahofu anaweza kuwa mtoto wa mitaani, alisema zaidi.
"Nawaambia
wanaume huko waliko waache kutubebesha mimba na kututelekeza, huyu
mtoto sijazaa na mzazi wangu nimezaa na wewe mwanaume uliyenikimbia,
yaani nina dukuduku natamani nimkamate huyo mwanaume nimkamue ili aone
uchungu wa maisha," alisema Mwajuma.
Awali,
kambi hiyo ilipangwa kufanyika kwa siku tatu lakini kutokana na wingi
wa wanawake waliojitokeza Makonda alitangaza iendelee kwa siku tano
mfululizo ili kuhudumia wengi zaidi.
Wanawake hao wanapewa msaada wa kisheria na wanasheria mbalimbali, polisi na maofisa wa ustawi wa ajamii.
No comments:
Post a Comment