Waziri
Mkuu wa zamani, Edward Lowassa amesema hamtambui mwanamke
aliyejitambulisha juzi kama binti yake aliyetelekezwa na kwamba
hatapoteza muda kwenda kupimwa vinasaba (DNA), kama msichana huyo
alivyotaka.
Kwa
mujibu wa mazungumzo na Gazeti la Nipashe, Lowassa ambaye kwa sasa ni
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),
alisema kuwa kinachofanyika kwenye zoezi hilo ni siasa.
Msichana
huyo aliyejitambulisha kwa jina la Fatuma alijitokeza hadharani juzi
katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na kudai kutelekezwa na
Lowassa ambaye alisema ni baba yake, kwa kuambiwa na mama yake mzazi.
"Wewe
unamwamini kweli huyo msichana? Angekuwa mwanangu kweli ningeshamchukua
muda mrefu, kwanza wala simjui naona siasa zinaingizwa hapo," alisema.
Alipoulizwa
kama yuko tayari kupimwa DNA ili ukweli ujulikane, Lowassa alijibu
"Kupima DNA huo ni upuuzi. Yaani nipoteze muda wangu kwenda kufanya
upuuzi huo? Siko tayari."
Msichana huyo ni miongoni mwa mamia ya wanawake waliojitokeza kuanzia Jumatatu kuitikia wito wa Mkuu wa Mkoa, Paul Makonda.
Makonda
alitaka wanawake waliotelekezewa watoto na waume zao wafike ofisini
kwake kwa siku tatu kuanzia Jumatatu, kwa ajili ya kuzungumza na
wanasheria, maofisa wa ustawi wa jamii na askari polisi wa Dawati la
Jinsia. Siku hizo zitaisha kesho baada ya kuongezwa.
Akizungumza
na vyombo vya habari juzi, Fatuma alisema yuko tayari kupima vinasaba
na Lowassa ili kuthibitisha kama kweli ni baba yake na kwamba alimtafuta
kwa muda mrefu bila mafanikio.
"Nilipeleka
barua Ikulu kuomba kuonana na baba (Lowassa) kipindi akiwa Waziri Mkuu
(2006-2008) lakini niliitwa mimi na mama katika klabu ya Mamba iliyopo
Kinondoni," alisema Fatuma.
"(Hapo) alikuja mwanaume akiwa kwenye gari lenye vioo vyeusi akatuhoji mimi na mama, akaondoka hakutupa majibu yoyote hadi leo."
Kuhusu madai hayo, Lowassa alisisitiza kuwa kama kweli angekuwa mtoto wake asingesita kumchukua.
"Wala
simjui, anasema ameshindwa kuniona wakati ana miaka 31, wewe unaamini
kweli ameshindwa kuniona? Mbona wewe umenitafuta na umenipata na
unaongea na mimi kwenye simu," alisema Lowassa.
"Hizo ni siasa zinazolenga kuchafuana."
Pia
katika maelezo yake, Fatuma alidai kuwa aliwahi kukutana na mtoto wa
Lowassa aitwaye Fred na alimwahidi kumsaidia lakini hadi sasa amekuwa
kimya.
No comments:
Post a Comment