Na Mathias Canal, WK-Simiyu
Waziri
wa kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba ametangaza kuwa maadhimisho ya
maonesho ya kilimo na sherehe za wakulima Nanenane Kitaifa yatafanyika
Mkoani Simiyu kwa miaka mitatu mfululizo kuanzia mwaka 2018 mpaka 2020
ili kuongeza tija ya elimu kuhusu sekta ya kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa
wananchi wa kanda ya Ziwa Mashariki.
Waziri
wa kilimo Mhe Tizeba ametanga neema hiyo kwa wananchi wa kanda ya ziwa
Mashariki jana tarehe 8 Agosti 2018 kwa wakazi wa mikoa ya Simiyu,
Shinyanga na Mara ambayo inaunda kanda ya ziwa Mashariki ambao
watanufaika na elimu kuhusu kilimo, mifugo na uvuvi.
Alisema
kuwa kumekuwa na utaratibu wa kufanyika mfululizo maonesho hayo kwenuye
mikoa inayoandaa huku akieleza kuwa utashi uliopo katika kanda hiyo ni
mkubwa ukilinganisha na maonesho ya Nanenane yaliyofanyika kwa miaka
minne mfululizo katika Viwanja vya Ngongo Mkoani Lindi.
Alisema
kuwa kufanyika mfululizo kwa miaka mitatu mkoani Simiyu kutawafanya
wananchi kuwa na uhakika wa bidhaa za uwekezaji watakazoziweka. “Mkoa wa
Simiyu na kanda yenu hii ya Magharibi ingetosha kuonyesha hata kwa
miaka miwili tu lakini nimeamua kutumia utaratibu mzuri zaidi ili
ifanyike kwa miaka mitatu naamini hamtaniangusha” Alikaririwa Mhe Dkt
Tizeba
Aliwataka
wakuu wa mikoa ya Shinyanga Mhe Zainab Telack, Mkoa wa Mara Mhe Adam
Malima na Mkoa wa Simiyu Mhe Antony Mtaka kuyafanya maonesho ya
Nyakabindi katika miaka miwili ijayo kuifanya sherehe hiyo ya Nanenane
kuwa ya kimataifa ili kuwe na washiriki kutoka katika nchi zote nane
zinazoizunguka Tanzania.
Alisema
kuwa ingependeza zaidi kuwa na washiriki wa maonesho ya teknolojia na
mambo mbalimbali ya kilimo kutoka katika nchi hizo za jirani ili
kubadilishana uzoefu katika kuinua sekta ya kilimo, Mifugo na Uvuvi.
Waziri
Tizeba alisema kuwa nchi ya Tanzania ndiyo kinara katikja kilimo katika
ukanda wa Afrika Mashariki na kati hivyo maonesho ya kilimo yanapaswa
kuwa katika mpango madhubuti wa kufikia maonesho ya kimataifa.
“Naomba
niwaahidi hapa kuwa sisi kama wizara tutatoa ushirikiano mzuri ili
kuhakikisha kuwa maonesho yajayo yanakuwa katika sura ya kimataifa kwani
kufanya hivyo tutakuwa tumeongeza ufanisi na elimu pana kwa wakulima
wetu wa chini” Alisisitiza Mhe Dkt Tizeba
Sambamba
na hayo pia Waziri wa kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba alimshukuru Rais
mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Benjamin Mkapa kwa
kukubali kuwa mgeni reasmi katika kilele cha maonesho ya Nanenane
Kitaifa kwani amekuwa chachu na hamasa katika kuongeza ufanisi na tija
kwenye sekta ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
Dkt
Tizeba alieleza kuwa kanda hiyo ya Ziwa Magharibi ya Nanenane
ilianzishwa kwa wazo la Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe Antony Mtaka ambaye
alitaka kutoa fursa ya urahisi wa hudua ya mafunzo kwa wananchi kufahamu
mbinu mbalimbali za kilimo, Ufugaji na Uvuvi.
MWISHO.



No comments:
Post a Comment