Serikali
inatarajia kutoa ajira 1,500 kwa askari wa kikosi cha zimamoto na
uokoaji kwa mwaka wa fedha 2018/19, ili kuondoa tatizo linalolikabili
pamoja na kutenga zaidi ya shilingi bilioni 4.5 kwa jeshi hilo ili
liweze kutoa huduma zitakazokidhi viwango vya kitaifa na kimatafa.
Akizungumza jana Agosti 29, 2018 katika wiki ya Jeshi la Zimamoto katika uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola alisema ajira hizo zitaongeza kasi ya kukabiliana na majanga ya moto yanayojitokeza maeneo mbalimbali nchini.
“Tunatambua
changamoto ya upungufu wa wafanyakazi katika kikosi hiki hivyo
tutaajiri watumishi 1,500 ili kuongeza nguvu iliyopo,” amlisema Lugola.
Katika
hatua nyingine, Lugola amewaagiza wakurugenzi wote wa majiji pamoja na
miji kutoruhusu ujenzi holela na badala yake wazingatie mipango miji kwa
sababu unasababisha vikosi vya zimamoto kushindwa kufika eneo la tukio
kwa wakati.
Kamishna
Jenerali wa jeshi hilo, Thobias Andengenye alisema wanakabiliwa na
uhaba wa wafanyakazi ikilinganishwa na ukubwa wa nchi na idadi ya
wananchi na kutaja changamoto nyingine kuwa ni upungufu wa magari katika
ofisi za mikoa na wilaya na kupendekeza magari 100 yatasaidia kufanya
kazi kwa urahisi.
Agosti
19 magari saba ya mizigo yaliteketea kwa moto katika kituo cha forodha
Rusumo wilaya ya Ngara, mpakani mwa Tanzania na Rwanda, baada ya gari
moja la mafuta ya petroli kuligonga gari jingine hali iliyopelekea
Helkopta ya jeshi la Rwanda kusaidia kuzima moto ulioteketeza shehena
iliyokuwa imepakiwa na magari hayo baada ya kukosekana kwa magari ya
zimamoto wilayani humo.






No comments:
Post a Comment