RAIS
wa China, Xi Jinping amesema China itatoa jumla ya dola bilioni 60 za
Marekani kwenye mpango wake wa miaka mitatu ya ushirikiano na Afrika
katika shughuli za maendeleo.
Ameyasema
hayo leo (Jumatatu, Septemba 03 ,2018) wakati akifungua Mkutano wa
Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) unaofanyika jijini
Beijing nchini China.
Rais
Jinping ameahidi kuwa nchi yake itatoa ushirikiano ili kuhakikisha
kwamba amani ya kudumu inapatikana Barani Afrika, hatua ambayo ni muhimu
kwa ustawi wa nchi za Afrika.
Maeneo
mengine ambayo Rais huyo ameahidi kuwa China italisaidia Bara la Afrika
ni pamoja na ujenzi wa miundombinu, ushirikiano katika sekta ya
biashara na huduma za afya.
Kadhalika,
Rais Jinping amesema China itatoa nafasi za mafunzo ya kilimo bora na
mafunzo ya ufundi kwa watalaam kutoka nchi za Afrika ili kuchangia
katika maendeleo ya uchumi.
Amesema
hivi sasa anaamini kwamba China na nchi za Bara la Afrika wako karibu
zaidi na wanashirikiana vizuri sana katika shughuli za kimaendeleo
ikilinganishwa na miaka ya nyuma.
Mkutano
huo ulianza kwa sherehe ya ukaribisho na baadae viongozi kutoka nchi
mbalimbali barani Afrika na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antyonio
Geterres walipata fursa ya kupiga picha ya pamoja na mwenyeji wao Rais
wa China.
Waziri
Mkuu, Kasim Majaliwa ambaye anamuwakilisha Rais Dkt. John Magufuli
katika mkutano huo alisalimiana na Rais Jinping baada ya ufunguzi.
Mkutano huo utaendelea kesho ambapo viongozi wengi kutoka Bara la Afrika
watapata nafasi ya kuzungumza.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATATU, SEPTEMBA 03, 2018.
No comments:
Post a Comment