Fahirisi
za Bei za Taifa ni kipimo kinachotumika kupima mabadiliko ya bei za
bidhaa na huduma mbalimbali zinazotumiwa na sampuli wakilishi ya kaya
binafsi nchini Tanzania. Bei za bidhaa na huduma 278 zikiwa ni pamoja na
bidhaa 97 za Vyakula na Vinywaji Baridi na 181 zisizo za Vyakula
hukusanywa kila mwezi katika kila mkoa.
Mizania Mpya za Bidhaa na Huduma na Jamii na Kizio cha Bei
Mizania
ya Fahirisi za bei za Taifa zimetokana na matumizi ya kaya binafsi
kutoka mikoa 25 ya Tanzania Bara. Mizania inajumuisha matumizi ya kaya
zote binafsi kutoka mijini na vijijini yaliyotokana na Utafiti wa Mapato
na Matumizi ya Kaya binafsi wa mwaka 2011/12. Kizio cha bei
kinachotumika kukokotoa Fahirisi za Bei za Taifa ni cha mwezi Desemba,
2015.
Makundi ya Bidhaa na Huduma za Jamii
Fahirisi
za Bei za Taifa hufuata makundi yaliyokubalika Kimataifa yanayoitwa
mchanganuo wa matumizi binafsi “Classification of Individual Consumption
by Purpose (COICOP)”. Fahirisi za Bei zinajumuisha makundi 12 ya mfumo
wa COICOP pamoja na fahirisi za bei kwa makundi maalumu. Makundi hayo
maalumu ni; 1) Vyakula na vinywaji baridi-vikijumuisha vyakula
vinavyoliwa majumbani na mahotelini; 2) Nishati na Mafuta - kundi hili
linajumuisha umeme na aina nyingine za nishati zinazotumika majumbani
pamoja na petroli na dizeli; 3) Fahirisi za bidhaa na huduma zote za
jamii isipokuwa vyakula na vinywaji baridi; 4) Fahirisi za Bidhaa na
huduma zote za jamii isipokuwa vyakula, vinywaji baridi, nishati na
mafuta.
Namna ya Kukokotoa Fahirisi za Bei za Taifa
Fahirisi
za Bei za Taifa katika ngazi za mwanzo hukokotolewa kwa kutumia wastani
wa jiometria “geometric mean of Price Relatives” na kanuni ya Lowe
Index Formula ambayo ni aina ya “Laspeyres Index Formula” hutumika
kukokotoa Fahirisi za Bei za Taifa katika ngazi ya makundi makubwa.
Mfumuko wa Bei wa Taifa kwa kipimo cha mwaka unapima kiwango cha kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma zote zinazotumiwa na kaya binafsi. Jedwali Namba 1 hapo juu linaonesha kuwa, Mfumuko wa Bei wa Taifa kwa mwaka ulioishia mwezi Agosti, 2018 umebaki kuwa asilimia 3.3 kama ilivyokuwa kwa mwaka ulioishia mwezi Julai, 2018. Hii inamaanisha kuwa, kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia mwezi Agosti, 2018 imebaki kuwa sawa na kasi iliyokuwepo kwa mwaka ulioishia mwezi Julai, 2018. Fahirisi za Bei zimeongezeka hadi 112.01 mwezi Agosti, 2018 kutoka 108.46 mwezi Agosti, 2017. Mfumuko wa Bei wa bidhaa za Vyakula na Vinywaji Baridi kwa mwezi Agosti, 2018 umepungua hadi asilimia 2.2 kutoka asilimia 2.8 ilivyokuwa mwezi Julai, 2018.
Mfumuko wa Bei kwa Bidhaa za Vyakula na Bidhaa Zisizo za Vyakula
Mfumuko wa Bei kwa kipimo cha mwaka kwa bidhaa za vyakula vinavyoliwa nyumbani na migahawani kwa mwezi Agosti, 2018 umeongezeka kidogo hadi asilimia 3.2 kutoka asilimia 3.0 mwezi Julai, 2018. Aidha, badiliko la Fahirisi za Bei kwa bidhaa zisizo za vyakula kwa mwezi Agosti, 2018 limeongezeka hadi asilimia 4.6 kutoka asilimia 4.2 mwezi Julai, 2018.
Mfumuko wa Bei wa Bidhaa na Huduma zote isipokuwa Bidhaa za Vyakula na Nishati
Mfumuko wa Bei ambao haujumuishi vyakula na nishati kwa mwezi Agosti, 2018 umeongezeka hadi asilimia 2.0 kutoka asilimia 1.6 mwezi Julai, 2018.
Fahirisi inayotumika kukokotoa aina hii ya Mfumuko wa Bei, haijumuishi vyakula vinavyoliwa nyumbani na migahawani, vinywaji baridi, petroli, dizeli, gesi ya kupikia, mafuta ya taa, mkaa, kuni na umeme. Vyakula na bidhaa za nishati vina sifa ya kuwa na bei ambazo hubadilika mara kwa mara, hivyo vikiondolewa kwenye fahirisi ya bidhaa na huduma zote hubakia fahirisi ambayo ina mwelekeo imara kwa Watunga Sera.
Kielelezo Namba 1 hapo juu kinaonesha kuwa, Fahirisi za Bei zimekuwa na mwenendo imara kutoka mwezi Agosti, 2017 hadi mwezi Agosti, 2018. Katika kipindi hicho, Mfumuko wa Bei umepungua kutoka asilimia 5.0 mwezi Agosti, 2017 hadi asilimia 3.3 mwezi Agosti, 2018.
MABADILIKO YA FAHIRISI ZA BEI KATI YA MWEZI JULAI, 2018 NA MWEZI AGOSTI, 2018.
Fahirisi za Bei kati ya mwezi Julai, 2018 na mwezi Agosti, 2018 zimepungua kwa asilimia 0.4 ikilinganishwa na kupungua kwa asilimia 0.3 mwezi Julai, 2018 kutoka mwezi Juni, 2018. Fahirisi za Bei zimepungua hadi 112.01 mwezi Agosti, 2018 kutoka 112.44 mwezi Julai, 2018.
Kupungua kwa Fahirisi za Bei kumechangiwa hasa na kupungua kwa bei za baadhi ya bidhaa za vyakula. Baadhi ya bidhaa za vyakula zilizochangia kupungua kwa fahirisi ni pamoja na; mchele kwa asilimia 1.7, mahindi kwa asilimia 3.6, unga wa mahindi kwa asilimia 3.5, unga wa ngano kwa asilimia 1.2, unga wa mtama kwa asilimia 2.0, mbogamboga kwa asilimia 2.8, mihogo kwa asilimia 1.6 na magimbi kwa asilimia 3.6.
No comments:
Post a Comment