Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa), Selemani
Jafo, ametoa miezi miwili kwa Wakala wa Majengo (TBA) kukamilisha
ujenzi wa ofisi za Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni zinazojengwa
katika eneo la Gezaulole.
Ujenzi
wa ofisi hizo ulianza Januari mwaka huu na ulitakiwa kukamilika Agosti
lakini hadi sasa haujakamilika na TBA wameomba kuongezewa muda hadi
Januari mwakani.
Akizungumza
jana baada ya kukagua ujenzi huo, alisema ofisi zinazotumika sasa ni
finyu na kumtaka mkandarasi huyo kukamilisha angalau gorofa moja ifikapo
mwishoni mwa Novemba ili ofisi zihamishwe.
“Haiwezekani
watu waendelee kukaa kwenye ofisi ambayo iko kama ‘briefcase’ hata
sehemu ya kusaini ni shida, naagiza mwishoni mwa mwezi wa 11 iwe jua iwe
mvua mkurugenzi na watumishi wako muwe mmehamia hapa,” alisema Jafo.
Naye
Mwakilishi wa TBA, Edwin Godfrey, alisema wameshindwa kukamilisha
ujenzi huo kwa wakati kwa sababu wakati wanaanza msingi walikumbana na
changamoto ya mvua.
Gharama ya ujenzi huo ni Sh bilioni 5.1 na hadi sasa TBA wameshapokea Sh bilioni 1.35.
Katika
hatua nyingine Waziri huyo aliipongeza manispaa hiyo kwa ujenzi wa
Kituo cha Afya Kimbiji lakini akawapa muda hadi ifikapo Novemba 30 mwaka
huu wawe wamekamilisha ujenzi wa jengo katika Kituo cha Afya Kigamboni.
Kwa
mujibu wa Jafo, manispaa hiyo ilipewa fedha za ujenzi huo Juni 26 mwaka
huu na kuagizwa hadi kufikia Oktoba 30 majengo yawe yamekamilika lakini
hadi sasa ujenzi haujaanza.
“Wakurugenzi wapya nendeni kwa kasi kubwa, nataka muwe mfano katika usimamizi wa miradi ya maendeleo.
“DED
(Mkurugenzi wa Halmashauri) Kakonko amejenga jengo zuri na tayari
limekamilika kwa Sh milioni 700. Pangani walipewa Sh bilioni 1.5 lakini
hata hawajui lini jengo lao litaisha,” alisema Jafo.
Naye
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, alisema wana changamoto
kubwa ya usimamizi na kumuomba waziri huyo kubadilisha mfumo wa wakuu wa
idara ili wawe wanapimwa kwa matokeo na si uzoefu wa kazi.
“Tumeshamwandikia
Waziri wa Utumishi ili wakuu wa idara waanze kuwajibika kulingana na
matokeo, wakurugenzi waanze kuwapima wakuu wao wa idara,” alisema
Makonda.
No comments:
Post a Comment