Na Mwandishi wetu, Washington
Chama cha Wanawake wa Afrika na
Uelewa wa Saratani (African Women Cancer Awareness Assossiation (AWCAA),
imemkabidhi Mke wa Rais Mama Salma kikwete, mashine moja ya Mammogram,
ambayo inatumika kupima ugonjwa wa saratani ya matiti, yenye thamani
ya zaidi ya dola za kimarekani laki mbili.
Makabidhiano hayo yalifanyika jana
katika ukumbi wa mikutano wa Ubalozi wa Tanzania uliopo Mjini
Washington D.C Nchini Marekani.
Akiongea mara baada ya kukabidhiwa
mashine hiyo, Mama Kikwete, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya
Wanawake na Maendeleo (WAMA), alikishukuru chama hicho kwa mashine
waliyowapatia wanawake wa Tanzania na kusema itaokoa maisha ya wanawake
wengi.
Alisema ugonjwa wa saratani ya
wanawake ambazo ni matiti na shingo ya kizazi, zinaua wanawake wengi
lakini wengi zaidi wanakufa kwa saratani ya shingo ya kizazi
ukilinganisha na magonjwa mengine kama maralia na Ukimwi
Mama Kikwete alisema,
“Tunaishukuru Serikali yetu kwa jitihada inazozifanya dhidi ya ugonjwa
huu, lakini bado utambuzi wa ugonjwa ni mdogo kwani bado kuna tatizo la
unyanyapaa miongoni mwa jamii jambo linalosababisha wanawake wenye
matatizo kuogopa kusema na hivyo kutambuliwa katika hatua ya mwisho ya
ugonjwa ambayo haina njia mbadala”.
Alisema WAMA kwa kushirikiana na
Chama cha Madaktari Wanawake Tanzania (MEWATA), wanafanya kazi ya
kuwaelimisha wananchi ili waweze kuutambua ugonjwa huo na wanawake
wameelekezwa jinsi ya kujipima wenyewe saratani ya matiti.
Pia madaktari kupitia kampeni
maalum wanaenda mikoani kuwapima wanawake ambao wakikutwa na matatizo
wanaandikiwa na kwenda kupata matibabu katika Hospitali za Rufaa za
Kilimanjaro, Mbeya na Bugando.
Mama Kikwete alisema, “Tatizo
lililopo mashine za Mammogram ni chache, wanawake wengi wanaoishi
vijijini hawawezi kusafiri na kwenda kupata huduma za matibabu kutokana
na ukosefu wa nauli lakini wakati wa kampeni za upimaji wanajitokeza
kwa wingi”.
Tunachotakiwa kufanya ni
kuhakikisha mashine zinapatikana kwa wingi pia jamii ikiondoa unyanyapaa
kila kitu kitawezekana kwani hivi sasa teknolojia imekuwa mtu
anatibiwa na kupona saratani hafi kama ilivyokuwa zamani”.
Akiongea mara baada ya kukabidhi
mashine hiyo Mwanzilishi wa AWCAA, Mama Ify Nwanbuku, alisema wanawake
wengi wa Afrika wanapoteza maisha kutokana na ugonjwa wa saratani kwa
vile hawana uelewa kuhusu ugonjwa huo na pia upatikanaji wa huduma za
matibabu ni mgumu.
Alisema kazi wanazozifanya ni
kutoa elimu kwa jamii kuhusu saratani ya matiti, kusaidiawanawake
takriban 100 kwa mwaka ili waweze kufanyiwa uchunguzi na kupata huduma
ya saratani ya matiti, kutoa huduma za kijamii kwa wagonjwa zikiwemo za
kifedha na misaada na kutoa misaada kwa watoto yatima ambao wazazi wao
wamefariki kwa saratani.
“Kwa kushirikiana na wadau
mbalimbali wa afya wa nchini Marekani tunafanya kazi hizi ndani ya
Marekani kwa kuwasaidia wanawake wenzetu wa kiafrika na pia katika nchi
za Afrika tunafanya kazi katika nchi za Sudani, Cameroon, Nigeria na
ninaamini siku moja tutakuja kufanya kazi nchini Tanzania ili tuweze
kuwasaidia na wenzetu wa huko.” alisema Nwanbuku.
Kwa upande wake Asha Hariz ambaye
ni Mwenyekiti wa kikundi cha wanawake wajasiriamali wa Tanzania waishio
nchini Marekani cha Wanawake watano (Tano Ladies) ambao ndiyo walisaidia
kupatikana kwa mashine hiyo alisema wanaamini mashine ya Mammogram
itasaidia kuokoa maisha ya wanawake nchini Tanzania ambayo ni moja ya
malengo ya WAMA.
Alisema nchini Marekani kuna watu
milioni mbili na laki tisa wanaishi na saratani hii ni baada ya
kujikinga mapema, kupata elimu ya saratani ya matiti na kufanyiwa
uchunguzi hivyo basi hata nchini Tanzania kama wanawake wenye saratani
watagundulika mapema na kupata matibabu wataweza kuishi muda mrefu .
Hariz alisema, “Tunaelewa kwamba
mgonjwa akipata huduma na kujikinga mapema hatakufa kwa sababu katika
jamii yetu kuna watu wanaoishi na saratani ya matiti kwa muda mrefu
ambao hivi sasa wanafanya kazi ya kuilelimisha jamii ili watu waweze
kupima na kuufahamu ugonjwa huu”.
Chama cha Wanawake wa Afrika na
Uelewa wa Saratani kilianzishwa mwaka 2004 kwa kushirikiana na wanawake
wa kiafrika wahamiaji na wataalamu wa afya kwa ajili ya kuondoa utofauti
katika uelewa, kujikinga na kupata huduma za Afra kwa jamii ya waafrika
wahamiaji wanaopata ugonjwa wa kansa.
Kikundi hicho kimekuwa na kuongeza
wataalamu wa afya, wajasiriamali na watu wanaoguswa na malengo ya
kikundi ya kutoa tofauti ndani ya wakazi wa Washington, Bara la Afrika
na Duniani kote.
No comments:
Post a Comment