KWA MAONI AU USHAURI E-mail: inocomm2014@gmail.com, PIGA SIMU: 0714555668

www.utt-pid.org


TEMBELEA: www.utt-pid.org

September 16, 2014

TUSHIRIKIANE KUONDOSHA MATUMIZI YA KEMIKALI ZINAZOHARIBU TABAKA LA OZONI.
Na Benedict Liwenga, MAELEZO-Dar es Salaam.
16/09/2014.
Tarehe 16 Septemba, mwaka huu Tanzania inaungana na Jumuiya ya Kimataifa katika kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Hifadhi ya Tabaka la Ozoni kama ilivyoagizwa na Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika azimio lake la 49/114 la tarehe 19 Desemba, 1994 huku kauli mbiu yake ikiwa ni ‘Ulinzi wa Tabaka la Ozoni; Jitihada zinazoendelea (Ozone Layer Protection; Mission Goes On)’.
Tarehe hiyo ni kumbukumbu ya kutiwa saini Mkataba wa Montreal (Montreal Protocol-1987) kuhusu kemikali zinazomonyoa Tabaka la Ozoni kwa kudhibiti utengenezaji na matumizi ya kemikali zinazoharibu Tabaka hilo.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) zinaeleza kuwa, Mkataba huo umepata mafanikio makubwa ya kupunguza zaidi ya asilimia 98% ambapo ni takribani tani milioni 1.8 ya uzalishaji na matumizi ya kemikali zinazomong’onyoa Tabaka la Hewa ya Ozoni.
Aidha taarifa inesema kuwa, punguzo hilo limechangia katika juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwasababu baadhi ya kemikali zinamong’onyoa tabaka la ozoni pia husababisha kuongezeka kwa joto duniani, mfano kiasi cha kemikali kilichoondolewa katika matumizi ni sawa na takriban tani bilioni 135 za hewa ukaa na hivyo kuchangia kwa kasi kubwa katika kukabiliana na ongezeko la joto duniani na mabadiliko ya tabianchi.
Matokeo ya tafiti yanathibitisha kwamba kiwango cha kemikali zinazoharibu tabaka la Ozoni angani kinaendelea kupungua na inakadiriwa kuwa iwapo jitihada za utekelezaji wa Mkataba huo zitaendelea, Tabaka la Ozoni litarudi katika hali ya kawaida ifikapo katikati ya karne hii.
Akizungumzia kuhusu mikakati ya kitaifa kwa ajili ya kufanikisha utekelezaji wa Mkataba huo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Mhe. Mhandisi Dkt. Mahenge alisema kuwa 1996 Serikali iliandaa na kutekeleza Programu ya Taifa ya kuondosha matumizi ya kemikali zinazomong’onyoa Tabaka la Ozoni, mikakati hiyo ni pamoja kujenga uwezo wa Taasisi zinazosimamia utekelezaji wa Mkataba, kuweka takwimu za kemikali hizo, kutoa elimu kwa wadau na kwa umma kuhusu umuhimu wa Tabaka la Ozoni na hatari zinazolikabili, kusambaza habari kuhusu kemikali na teknolojia mbadala, kubadilisha teknolojia katika viwanda vinavyotumia kemikali haribifu, kutoa mafunzo yanayolenga kuimarisha ujuzi katika sekta ya kuhudumia viyoyozi na majokofu.
Mikakati mingine ya kitaifa ni kuimarisha mbinu za upunguzaji wa matumizi ya kemikali husika kwa kuanzisha mtandao wa kunasa, kusafisha na kurejeleza vipoza joto, kuhamasisha na kuhimiza matumizi ya kemikali na teknolojia mbadala na rafiki kwa tabaka la Ozoni pamoja na kuweka taratibu za kudhibiti uingizaji na matumizi ya kemikali zinazodhibitiwa na Mkataba wa Montreal.
“Hatua hizi zimewezesha Tanzania kuondosha kemikali hizi kwa mujibu wa ratiba iliyowekwa na Mkataba”, alisema Dkt. Mwandisi Mahenge.
Dkt. Mahenge alibainisha kuwa Chini ya Programu ya Taifa ya kuondosha matumizi ya kemikali haribifu, serikali iliandaa Mpango wa Usimamizi wa Vipodozi yaani (Refrigerant Management Plan) na katika utekelezaji wake, mambo kadhaa yamefanyika ikiwemo kuandaa Kanuni za Usimamizi wa kemikali zinazomong’onyoa tabaka la hewa ya Ozoni ambazo zilianza kutumika tarehe 7 Desemba mwaka 2007.
Pia kusambaza kwa Vitambuzi vya kemikali hizo vipatavyo 18 kwa ajili ya vituo vilivyo mipakani mwa Tanzania, pia kusambaza mitambo na zana za kuhudumia majokofu na viyoyozi kama vile mashine za kunasa na kurejeleza gesi chakavu kwa vyuo vyote vinavyotoa mafunzo ya fani ya kuhudumia majokofu na viyoyozi hapa nchini.
Akivitaja vyuo hivyo vyenye kutoa mafunzo ya fani hizo, Dkt. Mahenge alisema kuwa kuna Vyuo vya VETA vilivyopo Chang’ombe jijini Dar es Salaam, Kihonda Morogoro, Moshi na Kigoma, YMCA, JKT-Mgulani, Vyuo vya uvuvi vya Mbegani-Bagamoyo na Nyegezi jijini Mwanza, Taasisi ya Taifa ya Usafirishaji, Chuo cha Teknolojia cha Dar es Salaam, Taasisi ya Teknolojia ya Karume Zanzibar, Taasisi ya Sayansi na Teknolojia-Mbeya pamoja na Chuo cha Mafunzo ya Ubaharia (DMI) kilichopo Dar es Salaam.
“Vituo vitano vya Kikanda vya kunasa na kusafisha gesi chakavu za Majokofu na Viyoyozi vimeanzishwa katika vyuo vya VETA vya Mwanza, Chang’ombe-Dar es Salaam, Kigoma, Mbeya na Mkokotoni-Zanzibar”, alitaja Dkt. Mahenge.
Dkt. Mahenge aliongeza kuwa Mtambo wa kunasa na kurejeleza kemikali umewekwa katika Kituo cha Tanzania cha Uzalishaji Bora na Teknolojia Endelevu (Cleaner Production Centre for Tanzania).
Katika utekelezaji huo uliofanywa na serikali, jumla ya Maofisa Forodha na Wasimamizi wa Sheria wapatao 400 wamepatiwa mafunzo kuhusu namna ya udhibiti wa kemikali zinazomong’onyoa Tabaka la hewa ya Ozoni na hadi sasa Tanzania imeweza kupunguza zaidi ya tani 216 sawa na asilimia 86% ya kiasi cha matumizi ya kemikali hizo, mwaka 1999.
Hapa nchini maadhimisho haya yanafanyika kwa njia ya uelimishaji umma kuhusu Tabaka la Ozoni, faida zake, madhara ya kuharibika kwa Tabaka hilo na matumizi salama ya bidhaa zenye kemikali rafiki kwa tabaka la ozone, hivyo kupitia vyombo mbalimbali vya habari elimu hiyo itasambazwa kwa jamii ili kuongeza ushiriki katika kutekeleza jukumu hilo muhimu la kuilinda sayari hii.
Bila shaka kila mmoja anatakiwa kuonyesha juhudi katika kupunguza na kuondosha madhara katika Tabaka la Ozoni yanayosababishwa na bidhaa mbalimbali tunazonunua na kutumia majumbani au sehemu za biashara.
Katika kuhifadhi Tabaka la Ozoni Mhandisi Dkt. Mahenge alisema kuwa kila mwananchi anatakiwa kushiriki kwa kuzingatia mambo mbalimbali yakiwemo;-
Kuepuka kuingiza nchini gesi zilizopigwa marufuku pamoja na vifaa vinavyotumia gesi haribifu kama vile majokofu na viyoyozi vilivyokwishatumika (mitumba) na vipya vinavyotumia gesi aina ya R11 na R12, kuingiza nchini vipoozi mbadala na rafiki kwa tabaka la Ozoni kama vile gesi aina ya R134a, R407, R404, R600 na R717, kununua bidhaa zilizowekwa nembo rasmi isemayo ‘Ozone friendly’ ikiwa na maana kuwa ‘sahibu wa Ozoni’ au ‘CFC-free’ ikiashiria kuwa haina wala haikutengenezwa na kemikali zinazomong’onyoa Tabaka la Ozoni.
Tahadhari nyingine ni kuepuka kutupa ovyo majokofu na viyoyozi chakavu ama vifaa vya kuzima moto vyenye kemikali zinazomong’onyoa Tabaka la Ozoni aina ya ‘CFCs’ na ‘halon’, pia kuepuka matumizi ya kemikali aina ya ‘Methyl bromide’ kufukizia udongo na badala yake ni vema kutumia mbinu mbadala na usalama pamoja na mbinu tungamanishi za udhibiti wa wadudu waharibifu yaani ‘Intergrated Pest Management’.
Mafundi wa majokofu na viyoyozi hawanabudi kuhakikisha kuwa wananasa na kutumia tena vipoozi (refrigerants) kutoka kwenye viyoyozi na majokofu badala ya kuviacha huru visambae anagani. Aidha, watoe elimu ya kutosha kwa wateja wao juu ya njia rahisi za kutambua uvujaji wa vipoozi kutoka katika majokofu na viyoyozi wanavyotumia.
-MWISHO-

No comments:

Post a Comment