#Awaalika kuzalisha nishati ya upepo na jotoardhi
WAZIRI MKUU, Mizengo Pinda, amefanya
mikutano na wawekezaji kadhaa ambao wanahudhuria mkutano wa uwekezaji Barani Afrika, ulioanza jana kwenye Jijini London, Uingereza.
Katika mikutano hiyo, Waziri Mkuu,
alikutana na Mwenyekiti wa Taasisi ya Africa Matters Limited, Baroness
Linda Chalker, na kujadiliana naye masuala yanayohusu utawala bora.
Pia alikutana wawakilishi wa
kampuni ya PriceWaterhouseCoopers (PwC), wakiongozwa na Bw. David Tarimo
(kutoka Tanzania), Bw. John Gibbs (Kanda ya Afrika) na Bi. Anne Eriksson
(Kanda ya Afrika Mashariki), na kuzungumza nao masuala ya nishati na gesi
asilia, miundombinu na upatikanaji wa rasilmali fedha (mobilisation of
resources).
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu
alikutana na mwanzilishi na mweneyekiti wa kampuni ya Invest Africa, Bw.
Robert Hersov, pamoja na wenzake wanne na kumweleza Waziri Mkuu nia yao
kuwekeza Tanzania kwenye maeneo ya usindikaji mazao, ujenzi wa maghala
ya kuhifadhia mazao na ufadhili wa miradi inayokubalika kiuchumi na
ambayo ni rahisi kupatiwa mikopo (bankable projects).
Naye Mtendaji Mkuu wa kampuni ya
Globeleq, Bw. Mikael Karlsson, ambapo alimweleza Waziri Mkuu haja ya
kampuni hiyo kuzalisha umeme wa upepo, kama njia mbadala ya kuongeza
nishati hiyo badala ya kutegemea gesi.
Akijibu hoja zao kwa nyakati
tofauti, Waziri Mkuu aliwaeleza wajumbe wa timu hizo kwamba Tanzania ni
mahali pazuri kwa uwekezaji lakini pia ni lazima pande zote mbili ziwe
makini ili kuhakikisha katika kila mradi inapatikana mizania sawia ya
maendeleo (win-win situation).
Akizungumza na Bw. Karlsson wa
kampuni ya Globeleq jana (Jumatatu, Oktoba 20, 2014), Waziri Mkuu
alisema, fursa ya kuzalisha umeme wa upepo iko katika mikoa ya Singida,
eneo la Makambako (Njombe), Katavi na Rukwa.
“Sasa hivi mbali ya upepo, mnaweza
pia kuangalia uzalishaji wa nishati inayotokana na jotoardhi
(geo-thermal) katika eneo lililopo kwenye Bonde la Ufa. Kati ya megawati
40,000 zinazotarajia kuzalishwa ndani ya eneo hili, megawati 5,000 ziko
kwenye Bonde la Ufa la Tanzania”, alifafanua.
Kampuni ya Globelec pia inamiliki pia mitambo ya SONGAS ambayo inazalisha umeme kwa kutumia gesi asilia.
Waziri Mkuu aliwasili jijini
London kuhudhuria mkutano wa wakuu wa nchi unaohusu uwekezaji barani
Afrika (The Global African Investment Summit – TGAIS) kwa niaba ya Rais
Jakaya Kikwete na ameshiriki mjadala huo pamoja na Rais John D. Mahama
wa Ghana, Rais Yoweri Museveni wa Uganda, Rais Paul Kagame wa Rwanda.
Waziri Mkuu amefuatana na Naibu
Waziri wa Fedha, Bw. Mwigulu Nchemba, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Mahadhi Maalim, Naibu Waziri wa Nishati na
Madini, Bw. Charles Kitwanga, Naibu Waziri wa Uchukuzi, Dk. Charles
Tizeba na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Bw. Said Mwambungu.
No comments:
Post a Comment