![]() |
| Ntagazwa |
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema sakata la
kuchotwa kwa fedha za umma zaidi ya Sh. bilioni 300 kutoka Akaunti ya
Tegeta Escrow katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), bado ni bichi iwapo
Waziri wa Fedha, Saada Mkuya na Katibu Mkuu wake, Servacius Likwelile na
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Prof. Benno Ndulu, hawatahojiwa
na kuwajibishwa.
Alisema vigogo hao wanapaswa kuhojiwa kuhusiana na wizi wa fedha
hizo kwa kuwa kutokana na nafasi zao walipaswa kuwa na taarifa wakati
fedha hizo zinaondolewa BoT na kwenda katika akaunti za watu
walionufaika na mgawo.
Pia, kimetaka wahusika wengine wanaodaiwa kuchota kiasi cha Sh.
bilioni 160 kati ya bilioni 306 kutoka akaunti hiyo na kuziweka katika
Benki ya Stanbic, hivyo kuitaka pia taasisi hiyo ya fedha kuwaorodhesha
wote walioweka fedha hizo huko ili waweze kuchukuliwa hatua kama
ilivyokuwa kwa walioweka katika Benki ya Mkombozi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam,
Mwenyekiti wa Bodi ya Udhamini ya Chadema, Arcado Ntagazwa, alisema
hatua ya kututwa kazi kwa aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo
ya Makazi, Prof. Anna Tibaijuka na kujiuzulu kwa aliyekuwa Nishati na
Madini, Prof. Sospeter Muhongo, haitoshi kufumbua wizi wa fedha hizo za
umma katika akaunti.
“Hatua madhubuti za kushughulikia ukwapuaji wa mabilioni ya
Shilingi katika akaunti ya Tegeta Escrow hazijakamilika na haziwezi
kukamilika bila kuhojiwa au kuwajibishwa kwa Gavana wa Benki Kuu, Prof.
Benno Ndulu, Waziri wa Fedha, Saada Mkuya, Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha,
Dk. Servacius Likwelile,” alisema.
Ntagazwa alidai kuwa taifa linaendeshwa kwa ubaguzi na upendeleo
huku viongozi wakubwa serikalini wakilindana na kwamba mambo hayo
yakiachwa yatazidi kuchochea mbegu za uhasama miongoni mwa jamii na
kuliangamiza taifa.



No comments:
Post a Comment