Rais Jakaya Kikwete akiwa katika picha ya pamoja na Baraza lake la Mawaziri. Picha na Maktaba
Na Mwandishi Wetu, Mwananchi
Dar es Salaam. Hali bado ni tete kwa mawaziri
wakati Rais Jakaya Kikwete akiwasiliana na viongozi waandamizi kabla ya
kutangaza mabadiliko ya Baraza la Mawaziri baada ya kuwa na vikao kadhaa
jana na vigogo katika kile kinachoonekana kupata ushauri.
Rais anatarajiwa kutangaza mabadiliko makubwa au
madogo wakati wowote, ikiwa ni utekelezaji wa maazimio ya Bunge la
Jamhuri ya Muungano
kuhusu sakata la uchotwaji fedha kwenye Akaunti ya
Tegeta Escrow kabla ya chombo hicho cha kutunga sheria kuanza vikao
vyake Jumanne ijayo mjini Dodoma.
Sakata hilo, lililohusu takriban Sh306 bilioni
zilizokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), lilisababisha Anna Tibaijuka
kuvuliwa uwaziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kutokana na
kubainika kuingiziwa Sh1.6 bilioni na mmiliki wa zamani wa Kampuni ya
IPTL iliyo na mkataba na Shirika la Umeme (Tanesco) wa kuizuia nishati
hiyo.
Profesa Sospeter Muhongo, ambaye ni Waziri wa
Nishati na Madini anatakiwa aondolewe kwa mujibu wa maazimio ya Bunge na
hivyo kuwapo kwa nafasi mbili ambazo Rais atalazimika kuziziba kwa
kufanya mabadiliko madogo au makubwa kwenye baraza hilo.
Kwa mujibu wa habari ambazo gazeti hili ilizipata
jana kutoka vyanzo mbalimbali, vigogo kadhaa wa Serikali waliitwa Ikulu
kwa ajili vikao ambavyo inaaminika kuwa vya kujadili jinsi ya kumaliza
sakata hilo, ambalo linafuatiliwa na wananchi na nchi wahisani.
Hata hivyo, wapashaji wetu hawakuweka bayana kuwa
vikao hivyo vinahusu kukamilisha kushughulikia sakata hilo lililogusa
mawaziri wa sasa na zamani, wanasheria wakuu wa Serikali, watumishi wa
umma na viongozi wa kidini.
Habari zaidi zinasema kuwa mkuu huyo wa nchi alikuwa na vikao tangu asubuhi.
Rais anatazamiwa kuondoka Jumapili kwenda nje ya nchi kwa safari za kikazi, kwa mujibu wa chanzo chetu cha habari.
Shinikizo kubwa kwa sasa ni kumwondoa Waziri
Muhongo, ambaye Rais Kikwete alisema Desemba 22 mwaka jana kuwa
amemuweka kiporo kwa “siku mbili au tatu” kusubiri uchunguzi, lakini
mwezi mmoja sasa hakuna uamuzi uliofanywa dhidi ya mtaalamu huyo wa
miamba.
Tayari wabunge wa vyama vya upinzani wameshaeleza
kuwa watamwondoa kwa nguvu mbunge huyo wa kuteuliwa na Rais iwapo
atarejea bungeni Jumanne wakati Mkutano wa 18 wa Bunge utakapoanza mjini
Dodoma, wakati mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali
(PAC), Zitto Kabwe amesema Bunge halitampa ushirikiano waziri huyo na
kwamba atakuwa na kazi ngumu wakati wa Bunge la Bajeti katikati ya
mwaka.
Profesa Muhongo anatuhumiwa kutoshughulikia vizuri
sakata la escrow na kusababisha Serikali ikose fedha kwa njia ya kodi.
Juhudi zake za kujitetea bungeni ziliishia kwa wabunge kutoa vielelezo
kadhaa kuthibitisha hoja za kuhusika kwake kwenye sakata hilo.


No comments:
Post a Comment