
Dar es Salaam. Gazeti la The EastAfrican limepigwa marufuku kusambazwa Tanzania, ikiwa ni miaka 20 baada ya kuanzishwa kwake kwa ajili ya kuandika habari za ukanda wa Afrika Mashariki.
Kwa mujibu wa barua iliyotumwa mwakilishi wa The
EastAfrican nchini, uamuzi huo umechukuliwa kwa sababu gazeti hilo
“limekuwa likisambazwa nchini bila ya kuwa na usajili, kinyume na
kifungu cha 6 cha Sheria ya Magazeti, Namba 3 ya mwaka 1976”.
Uongozi wa Nation Media Group, ambao unamiliki
gazeti la The EastAfrican, umeelezea hatua hiyo kuwa ni ya kushangaza na
isiyokubalika.
Barua hiyo ya Januari 21, 2015 inaagiza
kusimamishwa mara moja kwa uchapishaji na usambazaji wa gazeti hilo
nchini Tanzania ‘’hadi litakaposajiliwa rasmi na Msajili wa Magazeti,
Idara ya Habari’’.
Kabla ya kutolewa kwa barua hiyo, mwakilishi wa
gazeti hilo nchini, Christopher Kidanka aliitwa Jumatano na kuhojiwa na
mkurugenzi wa Idara ya Habari, ambaye pia ni msemaji wa Serikali, Assa
Mwambene.
Katika mahojiano hayo, Serikali ilieleza
kutofurahishwa na jinsi gazeti hilo linavyoripoti habari na uchambuzi
wake (zikiwamo safu za maoni).
Mwambene alilituhumu gazeti hilo kwa kuwa na
mtazamo hasi dhidi ya Tanzania. Alitoa mfano wa maoni ya hivi karibuni
ambayo yalikosoa msimamo wa Serikali kuhusu waasi wa Rwanda, FDLR
walioko nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kama mfano wa
mtazamo wa gazeti dhidi ya nchi.
Mwambene pia alielezea katuni iliyotoka kwenye
toleo la wiki hii la The EastAfrican, kuwa ilionyesha kutozingatia
utamaduni na kwamba ilionyesha kutomuheshimu Rais.
Matokeo yake, The EastAfrican halitakuwa likisambazwa hadi masuala ya kisheria yatakapotatuliwa.
Akizungumzia uamuzi huo wa Serikali, mwenyekiti wa
Bodi ya NMG Group, Wilfred Kiboro alisema sababu zilizotolewa na
Serikali zinashangaza kwa sababu gazeti hilo limekuwa likisambazwa tangu
miaka 20 iliyopita.
“Kwa hakika hawawezi kuamka leo na kututangaza
kuwa hatuko kihalali. Kama ingekuwa ni suala la kuweka sawa mafaili,
hilo halihitaji hatua za kikatili za kufungia gazeti,” alisema.
Alisema kwamba sababu halisi “ziko sehemu nyingine
“ na zinaweza tu kuhusishwa na msimamo ambao gazeti hilo, na mengine ya
kampuni NMG, limechukua katika kuripoti rushwa, wizi wa mali za umma na
utoaji duni wa huduma kwa watu wa Afrika Mashariki.CREDIT MWANANCHI


No comments:
Post a Comment