Mwenyekiti wa CCM wa tawi la Texas, Houston nchini Marekani, Simon Makangula (katikati). Picha ya Mtandano
Mwenyekiti wa CCM wa tawi la Texas, Houston
nchini Marekani, Simon Makangula amehukumiwa kifungo cha mwaka mmoja na
nusu jela na kulipa faini ya zaidi ya Sh92.4 milioni kwa kosa la
kughushi nyaraka za ulipaji wa kodi.
Makangula ambaye ni mmiliki wa kampuni ya kutoa
huduma za malipo ya kodi iitwayo Mshale Investment & Tax Service,
alihukumiwa Ijumaa katika Mahakama ya Wilaya na Jaji Gray Miller kwa
udanganyifu huo wa kuwasaidia wateja wake kughushi nyaraka za kodi ya
mapato, kwa mujibu wa tovuti ya click2houston.com.
Wakili wa serikali nchini humo, Kenneth Magidson
pamoja na Lucy Cruz, wakala maalumu wa kitengo cha uchunguzi wa makosa
ya kihalifu katika masuala ya mapato ya Marekani, kwa nyakati tofauti
waliiambia mahakama kuwa Makangula alimsaidia mmoja wa wateja wake
ambaye ni raia wa Marekani kutayarisha malipo ya kodi yasiyo halali.
Sambamba na kifungo cha mwaka mmoja na nusu, pia Makangula anatakiwa kulipa faini ya Dola 51,645 sawa na Sh92.4 milioni.
Oktoba 15, mwaka jana, Makangula alikiri kosa hilo
mbele ya hakimu Miller na kuwa malipo ya kodi hiyo yalikuwa na
udanganyifu katika vipengele kadhaa, yakiwamo katika makadirio na idadi
ya wategemezi wa mlipakodi, mambo yaliyosababisha hasara ya Dola 9,731
za Marekani (Sh17.3 milioni).
Pia, katika kesi hiyo, Makangula alikiri kuwa
alimsaidia mteja wake kughushi kuwa yeye ndiye mmiliki pekee wa biashara
hiyo, hatua iliyosaidia watu wengine, washirika wa mteja wake, wakwepe
kulipa kodi.
Kampuni ya Makangula inajishughulisha na huduma za
ulipaji wa kodi, uhasibu, mfumo wa ulipaji wa kodi za mapato, biashara
za ardhi, kodi za majengo na ushauri wa masuala ya kodi ya mapato.
Makangula, ambaye ni mwenyekiti wa tawi la CCM la
Texas, anawaongoza wajumbe tisa wa halmashauri ya tawi wanaoishi
Marekani na mara kadhaa ameonekana kwenye picha akiwa na viongozi
mbalimbali wa Serikali na CCM wanaotembelea Marekani.CREDIT MWANANCHI


No comments:
Post a Comment