![]() |
WAFANYABIASHARA wa Soko la Kariakoo jijini Dar es Salaam, wameandamana
hadi kituo cha Polisi cha Kati, wakidai wapewe taarifa wapi alipopelekwa
Mwenyekiti Taifa wa Jumuiya ya Wafanyabiashara, Johnson Minja.
Baadhi ya wafanyabiashara hao walifunga maduka yao jana na kuandamana
wakishinikiza kuachiwa huru kwa Minja, ambaye aliondolewa katika Kituo cha
Polisi Kamata bila taarifa rasmi.Maandamano hayo ya wafanyabiashara, yalikumbana na ulinzi mkali wa
askari nje ya jengo la Kituo cha Kati na kuishia nje.Hata hivyo, baadaye baadhi ya viongozi wao walifanikiwa kuingia na
kufanya mazungumzo na Naibu Kamishna Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Siro
(pichani) ambaye aliwaeleza kuwa Minja amepelekwa Dodoma, ambako ndiko iliko kesi
iliyomfanya akamatwe.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya wafanyabiashara kujaa maeneo
ya kituo hicho cha Polisi, Kamanda Siro alithibitisha kupata taarifa ya
maandamano hayo na pia kushikiliwa Minja na Jeshi hilo ambapo alisema
amepelekwa Dodoma na kwamba yuko salama.
“Ni kweli Minja amekamatwa lakini tukio lililomfanya akamatwe alilifanya
Dodoma, amesafirishwa kupelekwa huko ambako kesi yake iko na kesho atafikishwa
mahakamani,” alisema Kamanda Siro.Siro alilaani kitendo cha wafanyabiashara hao kufunga maduka na kufanya
maandamano ambayo ni kinyumwe cha sheria.“Wangenipigia simu tu na kuniuliza, lakini sio kufunga maduka na kufanya
maandamano, kitu walichofanya sio kizuri na kwasababu ni mara ya kwanza
tumewasamehe, Minja yupo salama ila amepelekwa Dodoma kwenye kesi yake ya
uchochezi,” alisema Siro bila kufafanua zaidi ni uchochezi wa aina gani.Akizungumza na gazeti hili, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya wafanyabiashara
Tanzania, Mchungaji Silver Kiondo alisema wamepewa maelezo ya kwamba Minja amepelekwa
Dodoma hivyo wameamua kuondoka eneo hilo la kituo cha Polisi Kati ili wajipange
kusafiri kwenda Dodoma kumtolea dhamana.“Baada ya kupata taarifa kutoka kwa Kamanda Siro kwamba Minja yuko
Dodoma, tumewatangazia wafanyabiashara walioko hapa na tumeamua kuondoka,”
alisema Kiondo huku wakiondoka wakiwa wameandamana, lakini bila kelele yoyote
wakielekea Kariakoo.Kiondo alisema jambo ambalo liliwashtua wafanyabiashara ni Minja
alikamatwa juzi na Polisi na alitakiwa kuchukuliwa maelezo akiwa na mwanasheria
wake.Lakini, jana asubuhi baadhi ya viongozi walifika wakiwa na mwanasheria
kituo cha Polisi Kamata alikokuwa, lakini hawakumkuta, wakaambiwa amepelekwa
Dodoma bila maelezo yoyote zaidi.Waliporudisha taarifa hizo kwa wafanyabiashara, waliamua kuja kituo cha
Kati kupata taarifa zenye uhakika, kama kweli amepelekwa Dodoma ambapo
wamethibitishiwa hilo na kuelezwa kwamba kesi yake inadhaminika wanaweza kwenda
kumdhamini.CREDIT: HABARI LEO



No comments:
Post a Comment