
Ndugu zangu,
Nimeupokea kwa matumaini uteuzi wa Rais kwa George Simbachawene kuwa Waziri wetu wa Nishati na Madini.
Nimemsikiliza
mara kadhaa George Simbachawene akijenga hoja ndani ya Bunge. Binafsi,
kwa kupima hoja zake, naamini kuwa Simbachawene amesimamia upande wa
wengi. Simbachawene, Mbunge wa Kibakwe na aliyepata kuwa Naibu Waziri
Nishati Na Madini , sio tu anaijua sekta hiyo, lakini, anajua vema jinsi
wananchi wa vijijini , kule Kibakwe na kwengineko Tanzania
wanavyosubiri kwa hamu wafikishiwe umeme wa gharama nafuu, kazi ambayo,
aliyemtangulia Simbachawene, Profesa Muhongo alikuwa akiendelea kuifanya
kwa ufanisi.
Simbachawene
anatambua, kuwa mwelekeo wetu kama nchi kwa sasa ni wa kiuchumi zaidi.
Na kimsingi ni mwelekeo wa dunia nzima. Na kwenye uchumi mkubwa ambao
unaweza kuitoa nchi haraka kutoka mahali ilipo na kupiga hatua za haraka
za kimaendeleo ni kwenye sekta ya nishati, inahusu madini ikiwamo gesi
na mafuta.(P.T)
Na nchi
yetu inaingia sasa kwenye uchumi wa gesi. Inahitajika sana duniani.
Hivyo, ghafla, wakubwa duniani wanatuzonga kwa namna nyingi kutaka
kunufaika na rasilimali tulizo nazo.
Na
pengine ifahamike, kwa wakubwa hawa duniani. Wizara nyeti wanayoiangalia
kwa karibu katika nchi yetu ni ya Nishati Na Madini. Hivyo, Waziri
mwenye dhamana kwenye Nishati na Madini, kwa wakubwa wa dunia, yumkini
ni Waziri Muhimu sana kuliko wengine wote.
Nina
mfano, jioni moja, nikiwa Dar es Salaam, nilipata kualikwa kwenye hafla
fupi nyumbani kwa Balozi wa nchi moja ya Kimagharibi. Mahala pale
kulikuwa na watu wengi, akiwemo tajiri Sir Andy Chande, alikuwepo pia
Profesa Baregu. Na mwalikwa mwingine alikuwa Profesa Muhongo. Ajabu ya
jioni ile, mtu pekee aliyetambulishwa na mwenyeji wetu juu ya uwepo wake
ni Profesa Muhongo, Waziri wa Nishati na Madini, Tanzania. Jambo hilo
linapigia mstari nilichokieleza hapo juu.
Hivyo,
tukifanya makosa tukamweka Nishati na Madini, Waziri au watendaji wenye
uchu wa mali na madaraka, basi, ni rahisi kwao kutuharakishia laana ya
rasilimali. Maana, ni rahisi wakageuka kuwa mawakala wa matajiri
wachache badala ya watumishi wenye kusimamia maslahi ya umma.
Na
hakika, Nishati na Madini ni kama eneo lililofukiwa mabomu ya ardhini.
Na makombora ya angani bado yameelekezwa kwenye Nishati na Madini.
Tayari kuanza kufyatuliwa muda ukifika.
Ndugu
yangu Simbachawene awe na tahadhari kubwa. Akibaki amesimama upande wa
wanyonge walio wengi, basi, ahesabu kuwa watakuwa nyuma yake hata pale
atakapoelemewa na wachache wenye kujali maslahi yao.
Hivyo, chonde Simbachawene, usiende Nishati Na Madini ukageuka kuwa ' Simba wa Makaratasi!"
Maggid Mjengwa,
Dar es Salaam.


No comments:
Post a Comment